1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maji yamezidi unga nchini Syria

Saumu Ramadhani Yusuf31 Januari 2012

Upinzani nchini Syria umeitangaza siku ya leo kuwa siku ya maombolezi na ghadhabu baada ya takriban watu 100 wengi wakiwa ni raia kuuwawa katika ghasia zinazoendelea nchini humo.

https://p.dw.com/p/13tpb
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa
Baraza la usalama la Umoja wa MataifaPicha: AP

Hali hiyo inajiri wakati baraza la usalama la Umoja wa mataifa likijiandaa kukutana kufikia uamuzi wake juu ya mzozo huo wa Syria.Jitihada chungunzima za kimataifa zinaendelea, kujaribu kuuziwia utawala wa Syria ukomeshe mauaji.

Baada ya ghasia za muda mrefu na umwagikaji wa damu sasa maji yamezidi unga nchini Syria na hali hiyo sasa imelilazimu baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuingilia kati na kujiandaa kutoa uamuzi wake. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kwa upande mwingine akiwa nchi jirani ya Jordan kwa ajili ya mazungumzo kuhusu amani ya mashariki ya kati amezungumzia matumaini yake kuhusu mkutano wa leo mjini New-York kwamba utazaa matunda haraka ili kufikia matarajio ya jamii ya Kimataifa.Kauli ya Ban Ki Moon inasema tunanukuu,

'' Zaidi ya watu 5000 wameuwawa,hali hii haiwezi kuendelea.Kwa maana hiyo mkutano wa baraza la usalama ni muhimu sana.Natumai kwamba wanachama wa baraza hilo mara hii watakuwa na mshikamano wa kuchukua hatua na kuzungumza kwa kauli moja''

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton anaongoza upande wa nchi za Magharibi katika kuibinya Urusi kuunga mkono hatua ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ya kutaka kumzuia Assad na utawala wake kuendelea kuwakandamiza wapinzani wake.Urusi inasema azimio la baraza la usalama dhidi ya Syria ni hatua itakayofungua njia ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Jumatatu ni siku ya ghadhabu na maombolezi Syria
Jumatatu ni siku ya ghadhabu na maombolezi SyriaPicha: Reuters

Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu 5400 wameuwawa nchini Syria katika kipindi cha miezi 10. Hata hivyo Urusi yenye kura ya turufu katika baraza la usalama la Umoja huo limekuwa likipinga azimio lililowasilishwa na Morocco na kupinga na Syria likimtaka rais Assad kukubali kusitisha vita na kuyakabidhi madaraka kwa makamu wake kabla ya kuundwa serikali mpya ya umoja wa kitaifa. Baraza la kitaifa nchini Syriaambao ni upinzani limetoa taarifa katika mtandao wa kijamii wa Facebook likiita siku ya leo kuwa siku ya maombolezo na ghadhabu kuwakumbuka waliouwawa katika ghasia hizi.Wafuasi wa dini zote wametakiwa kuunga mkono siku hii kwa kufanya sala maalum na pia kupiga kengele makanisani kwa ajili ya kuonyesha umoja katika harakati hizi.

Mwandishi: Saumu Yusuf

Mhariri: AbdulRahman