1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya Bernd Riegert juu ya uamuzi wa Urusi kusimamisha utekelezaji wa mkabata wa udhibiti wa silaha

27 Aprili 2007

Mpango wa nchi za jumuiya ya NATO juu ya kuweka mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora katika nchi za Ulaya ya Mashariki umeikasirisha Urusi kiasi kwamba rais wa nchi hiyo ameamua kusimamisha utekelezaji wa mkataba juu ya kudhibiti majeshi na silaha za kawaida barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/CHFL

Mpango huo wa Marekani wa kujenga mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora siyo tishio kwa Urusi wanasema wataalamu wa masuala ya kijeshi.

Hivyo basi waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleeza Rice hakukosea aliposema kuwa wasiwasi wa Urusi juu ya mpango huo upuuzi . Kauli ya waziri huyo ni sahihi ikiwa itazingatiwa katika msingi wa tathmini za kijeshi.

Lakini kisiasa, wasi wasi wa Urusi siyo jambo la kipuuzi.Mpango wa Marekani na madola mengine ya NATO unatumiwa na Urusi kwa shabaha za kisiasa. Kwa kuufungamanisha mpango huo na masuala mengine, lengo la Urusi ni kuzigawanya Marekani na nchi za NATO za bara la Ulaya.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani bwana Frank Walter Steinmeier amedokoa chambo katika ndoana ya Urusi. Bwana Steinmeier ameitaka Marekani ishauriane na Urusi juu ya mpango huo wakuweka ngao ya kujihami dhidi ya makombora. Waziri huyo anataka maswali yote yanayohusu mpango huo yajibiwe kwa uwazi.

Mapema mwaka jana nchi za NATO kwa ridhaa ya serikali ya Ujerumani zilipitisha uamuzi huo wa kujenga mfumo wa ulinzi dhidi ya hatari ya mashambulio ya makombora ya masafa mafupi na marefu yanayoweza kutokea Mashariki ya Kati.

Urusi inasema kuwa mpango wa Marekani na nchi zingine za NATO unatishia usalama wake. Lakini nchi hizo zimeialika Urusi ishiriki katika katika mpango huo. Mlango bado upo wazi, madhali hakuna jambo la kuficha.

Lakini Urusi imejibu kwa kusimamisha utekelezaji wa mkataba uliofikiwa mnamo mwaka 1990 juu ya kudhibiti idadi ya majeshi na silaha za kawaida barani Ulaya.

Urusi inalenga shabaha zinazoenda mbali.Nchi hiyo haitaki jirani zake waingizwe katika jumuiya ya NATO. Hivyo basi rais Putin anatumia mradi huo wa nchi za NATO kama mwao ili kujitoa kabisa kwenye mkataba juu kudhibiti viwango vya majeshi na silaha za kawaida barani Ulaya.Kwani mkataba huo unaiwajibisha Urusi kuondoa majeshi yake kutoka nchi jirani.

Marekani haiwezi kufanya jambo jingine , zaidi ya kuialika Urusi ishiriki katika mfumo wa ulinzi wa pamoja. Kwani inafahamika kwamba Urusi nayo inajenga ulinzi wake dhidi ya hatari ya makombora yanayoweza kutokea Iran,Pakistan ama China.

Huu siyo wakati wa kurejea nyuma katika vita baridi.Rais Putin wa Urusi anatambua hayo vyema.