1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaonya kuhusu tishio la nyuklia la Urusi

7 Oktoba 2022

Rais wa Marekani Joe Biden amevielezea vitisho vya Rais wa Urusi Vladimir Putin kutumia silaha za nyuklia kuwa vikubwa zaidi kuwahi kutolewa tangu mgogoro wa makombora wa Cuba.

https://p.dw.com/p/4HtEZ
USA | Präsident Joe Biden
Picha: Chip Somodevilla/Getty Images

Rais Joe Biden amesema Marekani inajaribu kuuelewa mfumo atakaotumia Rais Putin ili kuvimaliza vita hivyo huku akionya kwamba kiongozi huyo wa Urusi "hana mzaha anapozungumzia juu ya uwezekano wa matumizi ya silaha za nyuklia, za kibayolojia au kemikali, kwa sababu jeshi lake limedhihirika kutokuwa na ufanisi.

Biden amesema kwa mara ya kwanza tangu mgogoro wa Kombora la Cuba, sasa kumekuwepo tishio la moja kwa moja la matumizi ya silaha za nyuklia, ikiwa hali itaendelea kama ilivyo.

Katika mgogoro wa mwaka 1962, Marekani chini ya Rais John Kennedy na Umoja wa Kisovieti chini ya kiongozi wake, Nikita Khrushchev, walikaribia kutumia silaha za nyuklia kutokana na uwepo wa makombora ya utawala wa KiSoviet huko Cuba.

Soma zaidi: 

Tishio la nyuklia la Urusi

Russland | Videokonferenz Wettbewerb Lehrer des Jahres | Putin
Rais wa Urusi, Vladimir PutinPicha: Gavriil Grigorov/AP Photo/picture alliance

Putin, ambaye anasherehekea leo miaka 70 ya kuzaliwa kwake, ameonya kutumia njia zote zinazohitajika, ikiwa ni pamoja na matumizi ya nyuklia ili kuilinda ardhi ya Urusi, ambayo sasa anasema inajumuisha mikoa minne ya Ukraine aliyoinyakua kinyume cha sheria.

Kwenye mkutano wa jana huko Prague katika Jamhuri ya Czech, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amewataka viongozi wa Umoja huo kutoa awamu nyengine ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine, ikiwa ni pamoja na ufadhili zaidi wa silaha na vifaa.

Akihutubia jana mkutano huo wa Prague, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema ulaya ichukue hatua kuvimaliza vita vyake na Urusi:

"Katika siku 225 za vita kamili, tayari tumeonyesha kwamba Ulaya inaweza kushawishi suala la vita na amani. Lakini sasa, sote kwa pamoja tunapaswa kuchukua hatua ili kutumia mfumo wa kuvimaliza kabisa vita hivi, na kufikia kanuni ya amani".

Soma zaidi:Eneo la makazi huko Zaporizhzhia lashambuliwa na Urusi 

Ukraine yatoa wito kwa NATO

Wakati hayo yakiarifiwa, katika mkoa wa kaskazini mashariki mwa Kharkiv ambapo vikosi vya Ukraine vilikomboa eneo kubwa mwezi uliopita, Afisa wa polisi eneo hilo Serhiy Bolvinov amesema miili ya raia 534 wakiwemo watoto 19 ilipatikana baada ya askari wa Urusi kuondoka.

Ukraine Präsident Zelenskiy
Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskiyPicha: Valentyn Ogirenk/REUTERS

Rais Volodymyr Zelenskiy amesema majeshi ya Ukraine yamefanikiwa kuyakomboa kwa haraka maeneo zaidi haswa kusini mwa nchi wakati uvamizi wa Putin uliodumu kwa miezi saba ukiendelea.

Soma zaidi:Biden amuonya Putin dhidi ya shambulizi la nyuklia Ukraine 

Zelenskiy amesema pia kuwa Jumuiya ya kujihami ya NATO inapaswa kufanya mashambulizi dhidi ya Urusi ili kuzuia matumizi ya silaha za nyuklia.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amelaani kauli hiyo ya Zelenskiy na kuitaja kama "wito wa kuanzisha vita vingine vya dunia visivyotabirika na vitakavyokuwa na matokeo mabaya".