1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masoko yarudia kupata faida baada ya bunge la Ujerumani kupiga kura

30 Septemba 2011

Masoko ya hisa ya Ulaya na Marekani yamepanda tena baada ya bunge la Ujerumani kuunga mkono kwa kauli moja upanuzi wa mfuko wa eneo la mataifa ya euro wa uokozi pamoja na madaraka yake.

https://p.dw.com/p/12jQx
Sehemu ya bunge la Ujerumani lililopiga kura Alhamis ,29.09.11 mjini Berlin kuidhinisha upanuzi wa mfuko wa eneo la euro.Picha: dapd

Masoko ya hisa ya Ulaya na Marekani yamepanda tena baada ya bunge la Ujerumani kupiga kura kwa wingi mkubwa kupanua mfuko wa eneo la mataifa ya euro wa uokozi pamoja na madaraka yake. Baada ya wiki kadha za mjadala mjini Berlin juu ya iwapo kuyaokoa mataifa yaliyokumbwa na madeni katika umoja wa Ulaya, hususan Ugiriki, wabunge 523 wamepiga kura kuunga mkono ongezeko la mchango wa Ujerumani wa kile kinachojulikana kama chombo cha uthabiti wa kifedha katika umoja wa Ulaya kufikia kiasi cha euro bilioni 211. Wabunge 85 wamepinga na watatu hawakupiga kura. Hii inaifanya Ujerumani kuwa mwanachama wa 11 katika umoja wa sarafu ya euro kuunga mkono mfuko huo. Slovakia , ambako wabunge wamegawanyika kuhusu suala hilo, itapiga kura mwezi Oktoba. Mjini Athens wakaguzi wa mahesabu kutoka umoja wa Ulaya , benki kuu ya Ulaya na shirika la fedha la kimataifa IMF wamewasili nchini humo kuanza tena kazi ya kupitia upya juhudi za Ugiriki za upunguzaji wa deni lake , hatua waliyoisitisha mapema mwezi huu kutokana na kushindwa kwa nchi hiyo kufikia malengo yake. Mamia ya wafanyakazi wa umma nchini Ugiriki wameandamana dhidi ya kurejea kwa wataalamu hao pamoja na ubanaji matumizi ya serikali. Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou amesema kuwa nchi yake inafanya juhudi ambazo zinakaribia kuvuka uwezo wa kibinadamu. Papandreou ambaye amefanya ziara nchini Ujerumani siku ya Jumanne, anatarajiwa kwenda Ufaransa leo.