1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Magharibi na Kiarabu kuijadili Libya

9 Juni 2011

Mataifa ya Magharibi na yale ya Kiarabu yanakutana leo mjini Abu Dhabi kuzingatia kile ambacho afisa mmoja wa Marekani amekiita ''mwisho wa mchezo'' kwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi.

https://p.dw.com/p/11XJT
Kiongozi wa Libya, Kanali Mummar GaddafiPicha: dapd

Mkutano huo unafanyika wakati ambapo Jumuiya ya Kujihami ya NATO kwa mara nyingine ikiongeza mshambulizi yake makubwa ya anga mjini Tripoli.

NATO jana usiku iliushambulia mji huo mkuu, mashambulizi ambayo yanaelezwa kuwa makubwa zaidi tangu Umoja wa Mataifa ulipopitisha azimio la kuweka marufuku ya ndege kuruka kwenye anga ya nchi hiyo mwezi Machi mwaka huu.

Maelfu ya wanajeshi wa Kanali Gaddafi jana walisonga mbele kuelekea mji wa Misrata, wakiushambulia kwa makombora kutoka pande tatu na kuwaua kiasi waasi 12.

Mawaziri kutoka kundi linaloitwa mawasiliano ya Libya, ikiwemo Marekani, Ufaransa na Uingereza pamoja na washirika wa mataifa ya Kiarabu ya Qatar, Kuwait na Jordan, mwezi Mei walikubaliana kutoa msaada wa fedha kuwasaidia waasi katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe. Wanatarajia kuimarisha utekelezaji wa ahadi hiyo kwenye mji huo mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu hii leo.

NATO-Generalsekretär Rasmussen
Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh RasmussenPicha: AP

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen amesema jeshi la muungano lazima lijiandae kurejesha amani baada ya mzozo wa Libya. Mkuu huyo wa NATO amesisitiza kuwa hakuna kikosi cha muungano kitakachofanya mashambulizi ya ardhini.