1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matajiri waomba kutozwa kodi

Angela Mdungu
19 Januari 2022

Kundi la zaidi ya mamilionea 100 kutoka mataifa tisa ulimwenguni, sambamba na mashirika ya kimataifa hii leo, yametoa wito wa kuanzishwa kwa kodi ya utajiri kwa matajiri duniani

https://p.dw.com/p/45muY
USA | Mitglieder der Patriotischen Millionäre veranstalten in New York einen Protest am Tag der Steuererklärung
Picha: Brendan MCdermid/REUTERS

 Makundi yaliyotoa wito huo ni pamoja na lile la "Mamilionea wazalendo" na la "Mamilionea kwa ubinadamu". Kwa pamoja makundi hayo yametoa kauli ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa  yanayoendelea katika jukwaa la uchumi duniani la Davos.

Katika kuunga mkono pendekezo la mamilionea wanaotaka kuanzishwa kwa kodi hiyo ya utajiri, shirika la misaada ya dharura la Oxfam limesema, kodi hiyo itasaidia kupunguza ukosefu mkubwa wa usawa na kufadhili huduma muhimu za kijamii kama vile afya ya umma na elimu.

Kulingana na maelezo ya data za shirika la Oxfam, kodi hiyo ya utajiri inaanza na asilimia 2 pekee kwa mamilionea na inayoongezeka kwa asilimia 5 kwa mabilionea inaweza kukusanya dola za kimarekani trilioni 2.5 kwa mwaka.

Pendekezo la mabwanyenye hao limetolewa baada ya utafiti kuonesha kuwa kodi ya utajiri kwa watu matajiri zaidi duniani kwa mwaka inaweza kutosha kulipia chanjo dhidi ya virusi vya corona kwa kila mtu na kuwatoa watu bilioni 2.3 kwenye dimbwi la umasikini. Pamoja na hayo, kodi hiyo itatosha kutoa huduma za kijamii kwa takribani watu bilioni 3.6 katika mataifa yenye kipato cha kati na cha chini.

Utafiti huo ulifanywa na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali na makundi ya kijamii pamoja na shirika la Oxfam ambapo kundi la matajiri wazalendo pia lilishirikishwa.

Tutozeni kodi sisi, matajiri, na mtutoze sasa

Katika barua ya wazi kwa jukwaa la uchumi watu hao wenye utajiri mkubwa akiwemo mrithi wa kampuni ya Disney, Abigail Disney, imeelezwa kuwa mfumo wa sasa wa ukusanyaji mapato hauna usawa na umetengenezwa kwa mfumo ambao kwa makusudi, unawafanya matajiri kuwa na utajiri zaidi. Waliosaini barua hiyo ni matajiri wakiwemo wanawake na wanaume wa mataifa ya Marekani, Canada, Ujerumani, Uingereza, Denmark, Norway, Austria, Uholanzi na Iran.

Sehemu ya barua yao imeandikwa, kila nchi inapaswa kuwataka mabwanyenye walipe kiasi stahiki huku wakisisitiza "Tutozeni kodi sisi, matajiri, na mtutoze sasa"

Pendekezo hilo la kodi la leo, limetolewa wakati serikali mbalimbali duniani na wafanyabiashara wakubwa wakihudhuria mkutano wa Jukwaa la uchumi la Davos kwa njia ya video wiki hii baada ya mkutano wa ana kwa ana kuahirishwa kutokana na kuibuka kwa aina mpya ya virusi vya corona, Omicron.