1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Oxfam: Mabilionea watajirika maradufu wakati wa Covid-19

17 Januari 2022

Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la kimataifa la hisani la Oxfam imesema kuwa ukwasi wa watu 10 walio matajiri zaidi duniani umeongezeka marudufu katika muda wa miaka miwili ya mwanzo ya janga la virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/45c6J
Thema Frauenrechte in Lateinamerika | OXFAM | Yoana Galindo
Picha: IPDRS – OXFAM

Katika ripoti hiyo iliyotolewa kuelekea kuanza kwa mkutano wa kimataifa unaofahamika kama Ajenda ya Davos, shirika la Oxfam limesema kuwa utajiri wa watu hao 10 wanaofahamika kuwa na ukwasi mkubwa zaidi duniani umefikia dola za kimarekani trilioni 1.5 kutoka dola bilioni 700 miaka miwili tu iliyopita.

Kwa wastani takwimu hizo zinamaanisha mabwenyenye hao wamekuwa wakichuma kiasi dola bilioni 1.3 kila siku.

Kundi hilo la watu 10 ambao wote ni wanaume linajumuisha mmiliki wa kampuni ya kuunda magari ya umeme ya Tesla, Elon Musk, bilionea anayemiliki kampuni kubwa ya mauzo kupitia mtandao wa Amazon, Jeff Bezos na hata waanzilishi wa kampuni ya Google Larry Page and Sergey Brin. Wamo pia mmiliki wa kampuni ya Microsoft Bill Gates na yule wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mark Zuckerberg

Shirika la Oxfam limesema utajiri wa mabilionea hao umeongezeka zaidi wakati huu wa janga la Covid-19 kuliko ilivyokuwa miaka 14 iliyofuata baada ya anguko kubwa zaidi la kiuchumi duniani la 1929.

Oxfam: Wachache wanatajirika huku wengi wanakosa huduma muhimu

Berlin Tesla Gigafactory - Elon Musk
Mmiliki wa kampuni ya Tesla Elon Musk, moja ya mabilionea 10 duniani Picha: Patrick Pleul/dpa/picture alliance

Oxfam imeutaja ukosefu huo wa usawa kuwa "uhalifu wa kiuchumi" kwa sababu wakati watu 10 pekee wanaingiza mabilioni ya dola kila siku kuna watu wengine 21,000 wanakufa kila uchao kutokana na ukosefu wa huduma za afya, unyanyasaji wa kijinsia na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kufuatia ripoti hiyo Oxfam imependekeza serikali duniani kuchukua hatua nzito kukabili ukosefu mkubwa wa usawa kati ya walio nacho na wasio nacho. Moja ya mapendekezo ni kutoza kodi ya hadi asilimia 99 kwa faida yote iliyopatikana na mabilionea hao wakati wa janga la Covid-19

Mkuu wa shirika la Oxfam duniani Gabriela Bucher, amesema "Iwapo mmoja wetu angewatoza matajiri hawa kumi, kwa asilimia 99 kwenye faida waliyopata wakati wa janga la Covid-19, kiasi ambacho ni kikubwa kwa hakika, tungeweza kulipigia gharama zote za chanjo kwa ulimwengu mzima na kuwa na mifumo ya afya kwa kila mmoja. Tungeweza kufidia athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwa na sera za kupambana na ukatili wa kijinsia."

Shirika la Oxfam linatumai viongozi, watunga sera na wafanyabiashara watakaoshiriki mkutano kwa njia ya mtaandao wa Ajenda ya Davos unaoanza leo watatilia maanan yale yaliyoelezwa kwenye ripoti yao.

Brasilien | Coronavirus | Impfungen von Kindern
Ukosefu wa usawa katika ugawaji chanjo za Covid-19 ni moja ya changamoto zinazoikabili duniaPicha: Nelson Almeida/AFP/Getty Images

Hadi sasa takwimu zinaonesha janga la Covid-19 lililozuka mwishoni mwa mwaka 2019 limewatumbukiza watu milioni 160 kote duniani kwenye umasikini wa kutopea.

Oxfam imezisifu Marekani na China, madola mawili yenye nguvu za kiuchumi, kwa hatua inazochukua katika kurekebisha ukosefu wa usawa kwa kuongeza kiwango cha kodi kwa matajiri na kuidhibiti nguvu za makampuni makubwa yanayohodhi biashara duniani.