1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matatizo ya Umoja wa Mataifa kukusanya michango ya pesa

P.Martin12 Aprili 2008

Kila mwaka madola tajiri hutoa mabilioni ya Dola kwa Umoja wa Mataifa kusaidia kupambana na dharura za kibinadamu.Fedha hizo lakini hutolewa kwa mafungu na hivyo hukwamisha juhudi za umoja huo.

https://p.dw.com/p/DgVx
UN Secretary General Ban Ki-Moon, right, shakes hands with Liberia President Ellen Johnson Sirleaf upon arrival at the Valentino castle in Turin, Italy, Friday, Aug. 31, 2007, to attend a reunion of the UN representatives from all over the world. (AP Photo/Massimo Pinca)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.Picha: AP

Madola tajiri ndio yanazidi kushinikizwa kutoa mchango katika mfuko mmoja wa dharura,ili misaada iweze kutolewa kwa haraka na haki kwa nchi masikini na zilizokumbwa na maafa.Mito ya Umoja wa Mataifa kwa madola tajiri mara nyingi huitikiwa haraka zinapohusika nchi zinazovutia kisiasa au migogoro inayogonga vichwa vya habari duniani.Majadiliano hufanywa mara kwa mara kutafuta njia za kubadilisha utaratibu uliopo hivi sasa ambapo wafadhili hutoa kitita fulani tu kilichopangwa na hivyo dharura zinapotokea mashirika ya misaada yanalazimika kuomba michango zaidi.Utaratibu huo wa Umoja wa Mataifa huchelewesha huduma za misaada.Kwa hivyo mashirika yanayotoa misaada mara kwa mara hupaswa kurekebisha msaada unaoweza kutolewa na hata idadi ya wasaidizi watakaoajiriwa kugawa msaada huo.Pasipokuwepo mfuko wa fedha kwa ajili ya matumizi ya muda mrefu,ni vigumu kwa Umoja wa Mataifa kupitisha maamuzi na kutekeleza huduma zake.

Ni asilimia 50 tu ya Dola bilioni 15 zinazotumiwa kila mwaka na Umoja wa Mataifa kwa huduma mbali mbali, hutoka kwenye michango ya lazima ya wanachama wake 192.Malipo hayo ya kila mwaka huanzia Dola 14,000 kwa nchi maskini kabisa na kupindukia Dola milioni mia tatu na sitini na mbili zinazolipwa na Marekani.

Misaada ya kiutu ya ziada hutolewa kwa hiyari na hapo ndio kwenye shida.Kwani michango inayotolewa haitoshi kutekeleza misaada inayohitajiwa yanapotokea maafa ya kimaumbile au migogoro ya kibinadamu.Kwa mfano mwaka uliopita,Umoja wa Mataifa ulishindwa kupata hata nusu ya pesa zilizoombwa kukabiliana na maafa ya kimaumbile kama mafuriko ya Korea ya Kaskazini na vimbunga nchini Msumbiji.Na michango ya pesa kwa ajili ya migogoro inayoendelea Sudan na Somalia imetimizwa kwa theluthi moja tu.Isitoshe,shida zisizotazamiwa,kama kuongezeka kwa bei ya ngano na mazao ya maziwa hivi karibuni,ndio zimezidi kuongeza matatizo ya fedha ya Umoja wa Mataifa.

Lakini kwa maoni ya wafadhili,tatizo mojawapo kuu katika mfumo wa misaada wa Umoja wa Mataifa ni udhaifu wa utaratibu wake katika kueleza kiasi gani hasa huhitajiwa kupambana na maafa.Mfanyakazi mmoja wa Kingereza katika tume ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, amesema,hivi sasa kuna uhaba mkubwa kukusanya ushahidi wa kuwepo haja ya kutoa misaada ya kiutu na pia uwezo wa kukisia vipi misaada hiyo itaweza kufanikiwa.Kwa maoni yake utaratibu wa kutathimini mambo hayo unahitaji kurekebishwa ili Umoja wa Mataifa uweze kukusanya fedha zaidi kwa ajili ya maafa ya dharura na migogoro ya duniani.