1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mateka wa Korea Kusini waachiliwa huru Afghanistan

Maja Dreyer29 Agosti 2007

Kwa muda wa wiki sita, jamii mbalimbali ulimwenguni walikuwa na wasiwasi mkubwa juu ya Wakorea Wakristo ambao walitekwa nyara tarehe 18 Julai na wanamgambo wa Taliban. Hatimaye lakini leo kuna habari nzuri, kwamba Wataliban walianza utaratibu wa kuwaachilia huru mateka hawa.

https://p.dw.com/p/CB1e
Mwanamke wa Korea baada ya kuachiliwa huru
Mwanamke wa Korea baada ya kuachiliwa huruPicha: AP

Tangu siku kadhaa uvemi kuhusu makubaliano mapya kati ya wajumbe wa Wataliban na serikali ya Korea Kusini ulizagaa mjini Kabul, Afghanistan, lakini hatimaye leo tu habari hizo zimethibitishwa. Kulingana na makubaliano haya, mateka wote 19 wa shirika la Kikristo la Korea Kusini la kutoa misaada wataachiliwa.

Tayari mateka 12waliachiliwa huru. Kwa mujibu wa mzee Haji Mohammed Zahir ambaye akiwakilisha serikali ya Afghanistan alihudhuria majadiliano kati ya Wataliban na Wakorea, leo asubuhi matekahao wa kike walipelekwa kwake katika jimbo la Kaskazini Mashariki la Ghazni. Wako salama lakini wamechoka sana alisema Mzee Haji na akaongeza kueleza kwamba wanawake hawa wanashughulikiwa na shirika la msalaba mwekundu na wajumbe kutoka Korea.

Baadaye leo hii, mateka wengine tisa waliachiliwa katika sehemu mbali mbali za Agfanistan. Msemaji wa Wataliban alithibitisha kuwa mateka wote wataachiliwa, lakini kwa vile wako kwenye mahala tofauti utaratibu mzima utachukua siku kadhaa.

Korea Kusini kwa upande wake iliwaahidi Wataliban kuwa itawarudisha nyumbani wanajeshi wake 200 hadi mwisho wa mwaka huu. Lakini tayari kabla ya utekaji nyara, Korea ilipanga kuliondosha jeshi lake lenye wahandisi na madaktari. Juu ya hayo, serikali ya Korea Kusini iliahidi hakutakuwa tena kundi la wamisionari kutoka Korea Kusini nchini Afghanistan. Pia, tangu kisa hicho kutokea, nchi hiyo imepiga marufuku safari za wananchi kwenda Afghanistan. Kwa mujibu wa msemaji wa Korea Kusini, malipo ya kuwakomboa mateka hayakuzungumziwa.

Makubaliano haya yalifikiwa jana mjini Ghazni ambapo wajumbe wa serikali ya Korea Kusini na wawakilishi wawili wa Wataliban walikutana katika ofisi ya shirika la hilali nyekundu. Kabla ya mazungumzo haya, Wataliban walidai wafungwa wenzao waachiliwe kutoka gerezani. Serikali ya Afghanistan lakini ili kataa kukubali dai hilo.

Wataliban waliwateka Wakorea 23 hapo Julai. Wawili waliuawa na wanawake wengine wawili wagonjwa waliachiliwa baada ya mazungumzo kuanza.

Hadi sasa lakini, hakuna habari mpya juu ya mhandisi Mjerumani na wenzake wanne wa Afghanistan waliotekwa nyara siku moja kabla ya Wakorea. Kulingana na waziri wa ulinzi wa Afghanistan, watekaji walitaka kufuatilia mazungumzo kati ya Wataliban na Wakorea.

Wakati huo huo, mapigano kati ya jeshi la kimataifa na wanamgambo wa Taliban yanaendekea. Jana, wapiganaji wa kundi la Taliban wasiopungua 100 waliuawa kwenye mapigano jimboni Kandahar, Kusini mwa nchi hiyo, na wanajeshi watatu walikufa baada ya mshambuliaji aliyejitoa muhanga kujiripua karibu na kazi za ujenzi wa daraja inayofanywa na jeshi la NATO katika eneo la Mashariki.