1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji yaendelea nchini Somalia, likisubiriwa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika

Mohammed Abdul-Rahman27 Februari 2007

Hali nchini Somalia bado ni tete. Wanajeshi wa Ethiopia walioisaidia serikali ya mpito kuwan´goa madarakani viongozi wa mahakama za Kiislamu, wanajikuta wakiwa na maadui zaidi badala ya marafiki. Hali hiyo inatokana na hujuma zinazoendelea siku baada ya siku katika mji mkuu-Mogadishu.

https://p.dw.com/p/CHJH
Gari likiwaka moto baada ya kushambuliwa na kuripuka mjini Mogadishu na kuwauwa watu wanne waliokuwemo ndani ya gari hilo.
Gari likiwaka moto baada ya kushambuliwa na kuripuka mjini Mogadishu na kuwauwa watu wanne waliokuwemo ndani ya gari hilo.Picha: AP

Takriban kila siku wanajeshi wa Ethiopia na washirika wao waliopata mafunzo kabambe ya kijeshi, hujikuta wakishambuliwa kwa makombora,mizinga na risasi. Katika hali kama hiyo, raia pia wasio na hatia huuwawa baada ya kujikuta katikati ya mapigano.

Serikali ya mpito nchini Somalia inawatwika dhamana wanaharakati wa Kiislamu iliowan´goa kutoka mji mkuu Mogadishu na maeneo mengine ya kusini mwa nchi hiyo mwishoni mwa mwaka ikisaidiwa na wanajeshi wa Ethiopia.

Wachambuzi na wanabalozi wa nchi za magharibi wanasema bila ya kuudhibiti mji mkuu Mogadishu na kuanza mazungumzo ya upatanishi wa kitaifa, hakuna litakalobadilika.

Akitoa mfano wa uwezekano wa kupatikana mafanikio endapo hilo litafanyika, afisa mmoja wa kibalozi wa magaharibi aligusia juu ya mazungumzo yaliyoleta maelewano katika Jamhuri ya Somaliland, eneo lililojitenga la kaskazini mwa Somalia na pia katika mkoa wa Puntland, na kwamba hiyo ndiyo njia ya kuweza kusonga mbele panapohusika na Somalia.

Serikali ya Rais Abdilahi Yussuf Ahmed ni ya 14 katika jaribio la kuwa na utawala katika taiofa hilo, tangu alipoangushwa dikteta Mohamad Siad Barre 1991 na Somalia kuingia katika vurugu na vita . Tangu kuangushwa Siad Barre, masilahi ya koo yametawala zaidi kuliko yale ya taifa, na kugeuka kikwazo kwa serikali zilizoundwa hapo kabla.

Serikali ya mpito sasa inaanza ya kuanza mazungumzo ya upatanishi na kuleta umoja wa taifa, lakini kwanza inawajibika kuidhibiti hali ya mambo katika mji mkuu, kwani bila ya hivyo hakutokua na hali ya kuaminiana kuweza kuitishwa kongamano la aina hiyo.

Baadhi ya wadadsisi wanaamini hiyo ndiyo njia pekee , huku mmoja wao akisema “ ni utamaduni wa wasomali kukaa pamoja chini ya mti na kutatua matatizo yao.”

Katika kuleta usalama, serikali inategemea msaada wa jeshi la umoja wa Afrika-AU litakalochukua nafasi itakayoachwa na majeshi ya Ethopia ambayo yanapaswa kuondoka mara wanajeshi 8,000 wa umoja wa Afrika watakapowasili Somalia. Hadi sasa ni nusu tu ya ahadi iliotolewa. Ni Uganda, Burundi, Nigeria na Ghana zilizotangaza kuwa tayari kuchangia, huku Uganda ikisema itatuma wanajeshi 1,500 hivi karibuni, wakati Burundi imaeahidi kupeleka wanajeshi 1,700.

Wengi wanaamini Umoja wa Afrika utakua na changa moto kubwa kujaribu kuleta utulivu mjini Mogadishu kutokana na kushindwa kwa ujumbe sawa na huo kufanya kazi katika harakati za kuweka amani katika jimbo la magharibi mwa Sudan Darfur.

Kwa wakati huu matumizi ya nguvu yanaendelea. Leo shemeji wa Waziri mkuu Ali Mohamed Gedi alipigwa risasi na kuuwawa na watu waliokua nma silaha, akiwa miongoni mwa watano waliouwawa katika saa 24 zilizopita.

Watu wanne waliojizatiti kwa silaha walimfuata Yussuf Mohamed Dhisow ambaye ni mfanya biashara , wakati akitoka nyumbani kwake kaskazini mwa Moagadishu, kabla ya kulipita kwa kasi gari lake na kumiminia risasi. Dhisow ni mumewe dada wa waziri mkuu Gedi, Ayan Mohamed Gedi na familia yake ilisema aliuwawa katika soko kubwa la Bakara. Haikuweza kufahamika nani alikua nyuma ya mauaji hayo.

Mtaalamu mmoja wa masuala ya kijeshi, aliuonya kwamba kushindwa kwa jeshi la umoja wa Afrika litakalotumwa Somalia , kutaifanya hali ya mambo iwe mbaya zaidi, akiongeza kuana kitisho cha kushuhudiwa” Baghdad nyengine nchini Somalia.”