1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa nje wa Umoja wa Ulaya

9 Desemba 2009

Washindwa kuafikiana juu ya hatima ya Jeruselem ?

https://p.dw.com/p/Ky1i
Ger Guido Westerwelle na rais Peres wa Israel.Picha: AP

Mawaziri wa nje wa Umoja wa Ulaya, walijadiliana kwa masaa kadhaa jana juu ya azimio lao kuhusu hatima ya mji wa Jeruselem .Hii imedhihirisha kwamba, linapozuka swali la Mashariki ya Kati, Umoja huo unabidi kuchukua hadhari,kwani ni swali nyeti. Kimsingi, ilikua ni kuamua hapa ni eneo gani la jiji hilo liwe chini ya Mamlaka ya dola la Wapalestina,linalopangwa kuundwa.Kwamba, wapalestina waunde dola lao wenyewe, ni dai lilililotolewa kitambo na Umoja wa Ulaya na mada hiyo haina utata hata hivi sasa:

"Tunataka amani ya kudumu itakayo jengeka juu ya msingi wa suluhisho la dola mbili na kwa hivyo, tunahitaji haraka kama iwezekanavyo, kuanza mazungumzo ya moja kwa moja .Tunaunga mkono juhudi za kimataifa zinazolenga kuifikia shabaha hiyo na tunataka kutoa mchango wa nchi za ulaya upande huo."

Lakini, mchango wao Umoja wa ulaya , unabainika ni wa kusitasita.Kimsingi, ni wazi tangu miaka mingi ni mkondo gani wa kufuatwa:Mwambao wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ni mali ya wapalestina,lakini sio tu maeneo hayo pekee.

Mzizi wa fitina , unabakia jiji la Jeruselem.Je, jiji hilo litagawanywa na sehemu yake ya Mashariki kuwa mji mkuu wa dola la wapalestina ?

Na katika kutoa jibu juu ya swali hili jana, Umoja wa Ulaya , ulishindwa kutoa msimamo wake wazi.Awali,Sweden kama mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya, ilipendekeza kuwa Umoja wa Ulaya uamue hivyo kuwa sehemu moja ya jiji hilo iwe jiji kuu la wapalestina.Sweden lakini, imetiwa munda na kuangushwa katika msimamo wake huo.Wengi, miongoni mwao waziri wa nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, walihisi kuchukua msimamo huo ni kuvuka mpaka:

"Hatuwezi kulazimisha kukamlishwa kabisa mazungungumzo kwa kuchora kabisa mipaka dola la kipalestina ."

Westerwelle, wakati wa ziara yake ya hivi karibuni nchini Israel,aliikosoa Israel kwa sera zake za ujenzi wa maskani za wayahudi.Hivi sasa, inachagizwa mno kukomesha kabisa kujenga majumba ya walowezi katika ardhi za wapalestina na kuanza mazungumzo ya amani na wapalestina.

Umoja wa Ulaya ,hauna azma lakini ya mpambano wa uso kwa uso na Israel.Umoja wa Ulaya , umetakiwa na waziri wa nje wa Luxemburg,Jean Asselborn, uishinikize zaidi Israel na utoe madai yake wazi kwa Israel:

Uongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels,ulikanusha ila zilizotolewa kwake kwamba, haiambii Israel wazi.Waziri wa nje wa Sweden, Carl Bildt, akasema msimamo wa UU utachangia mno utaratibu wa amani katika mashariki ya Kati.

Mwishoe, Umoja wa Ulaya unaelewa kwamba, katika kuamua hatima ya mzozo huo, hawana turufu ya mwisho.Dola lenye ushawishi mkubwa ni Marekani.

Mtayarisi: Ramadhan Ali

Uhariri: Abdul-Rahman