1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MGOGORO WA MADENI, BARROSO ATAKA MJADALA

Abdu Said Mtullya5 Agosti 2011

Barroso ataka mjadala juu ya mgogoro wa madeni.

https://p.dw.com/p/12BZI

Rais wa Hamashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso amependekeza mjadala juu ya kuongeza fedha katika Mfuko unaotumika kwa ajili ya kuziokoa nchi zinazokabiliwa na migogoro ya madeni.

Bwana Barroso ametoa pendekezo hilo kutokana na shinikizo la mgogoro wa madeni linaloendelea barani Ulaya.

Katika Barua aliyoiandika kwa wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Ulaya Barroso ametoa mwito wa kuongeza fedha katika mfuko huo ambao sasa una Euro Bilioni 440. Lakini Ujerumani tayari imeshalipinga pendekezo hilo.

Wakati huo huo Benki Kuu ya Ulaya imeanza tena kuzinunua hati za dhamana za serikali za nchi zinazokabiliwa na migogoro ya madeni ili kuyatuliza masoko ya fedha. Kwa mara ya mwisho Benki hiyo ilichukua hatua hiyo mienzi minne iliyopita.

Hatua ya Benki Kuu ya Ulaya inafuatia kupanda sana kwa riba za dhamana za Italia na Uhispania mnamo siku zilizopita. Kupanda kwa riba hizo kumesababisha hofu ya kuenea kwa mgogoro wa madeni.