1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Mynmar waendelea

28 Septemba 2007

Wanajeshi na polisi nchini Mynmar leo wametumia virungu kuvunja maandamano ya wapinzani waliokuwa wanajaribu kukusanyika mjini Yangon.

https://p.dw.com/p/CB0s
Watu wakiabudu nchini Mynmar
Watu wakiabudu nchini MynmarPicha: AP

Wakati huo huo baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa baada ya kufikia kiwango cha uwakilishi kinachohitajika , limeamua kuitisha kikao maalum kujadili mgogoro wa nchi hiyo jumanne ijayo.

Msemaji wa baraza hilo bwana Gomes ameeleza kuwa majadiliano ya faragha yanafanyika kwa lengo la kupata azimio juu ya hali ya haki za binadamu nchini Mynmar.

Baraza hilo limeamua kuitisha kikao hicho baada ya majeshi na polisi ,leo vilevile kutumia nguvu kuwatawanya waandamanaji na kufyatua risasi angani ili kuwaonya.

Mgogoro wa Mynmar umeshasababisha vifo vya watu wasiopungua 13 tokea utawala wa kijeshi wa nchi hiyo uanze kuchukua hatua dhidi ya wapinzani wanaoongozwa na watawa wa kibudha.

Watu walioshuhudia wamesema kuwa maalfu ya wapinzani walikusanyika karibu na nyumba moja ya watawa na kuanza kuwashambulia askari kwa mawe.

Katika matukio ya leo watawa wanne walikamatwa na nyumba mbili za watawa nje ya mji mkuu Yangon zilikaliwa na majeshi.

Habari zinasema wanajeshi wamezifunga nyumba kadhaa za watawa zilizokuwa sehemu muhimu za upinzani mkubwa usiokuwa na mithili katika kipindi cha miaka 20 iiyopita.

Habari zaidi kutoka Yangon zinasema kuwa barabara zote muhimu za mjini huo zimewekewa vizuizi na , askari wanaendelea kuvisogeza vizuizi hivyo katika sehemu za kati za mji huo.

Utawala wa kijeshi wa Mynmar umeshutumiwa na viongozi mbalimbali duniani. Rais Bush ameulaani utawala huo kwa kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji na ameitaka China iwashinikize viongozi wa kijeshi wa utawala huo.

Umoja wa nchi za Asia Asean umeshutumu matumizi ya nguvu.Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo wametoa shutuma hizo kwenye mkutano wao mjini New York.

Kutokana na shinikizo la jumuiya ya kimataifa utawala wa kijeshi wa Mynmar umemruhusu mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa bwana Ibrahim Gambari kufanya ziara nchini humo.

AM.