1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 5 tangu kuasisiwa Umoja wa Afrika

9 Julai 2007

Mkuu wa idhaa ya Kiamharic ya Redio hii ya Deutsche Welle, Ludger Schadomsky, ambaye amefuatilia kwa muda mrefu siasa za Kiafrika, anachambua historia na mustakabali ya Umoja wa Afrika.

https://p.dw.com/p/CHBK
Mbele ya makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Abeba
Mbele ya makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis AbebaPicha: DW /Maya Dreyer

Umoja wa Afrika uliasisiwa kwenye mkutano maalum uliofanyika mjini Durban, Afrika Kusini, tarehe 8 hadi 10 Julai mwaka 2002, na unachukua nafasi ya Umoja wa nchi huru za Afrika, OAU. Umoja wa Afrika umeanzishwa na matiafa 52 kwa ujumla, yaani nchi zote za bara la Afrika ila tu Marokko. Uanachama wa Madakaskar ulisimimishwa kwa muda hadi mwaka 2002, na Mauretania imeondoshwa kwa muda kutoka Umoja wa Afrika baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 2005.

Kabla ya hapo, kiongozi wa Libya, Muammar al-Gaddhafi amependekeza uanzishwe Umoja wa Afrika, kuiga mfano wa Umoja wa Ulaya. Katika hati ya Umoja huu mpya nchi za Kiafrika zinajiwekea msingi wa kuimarisha demokrasia na Umoja wa nchi za Kiafrika, kuheshimu haki za binadamu, kupambana kwa pamoja na mizozo na kubeba jukumu kwa pamoja wakati wa vita. Baada ya nchi nyingi kuuidhinisha mkataba, mwaka 2001 kilianza rasmi kipindi cha miaka miwili cha kubadilika kutoka Umoja wa nchi huru za Kiafrika, OAU, kuwa Umoja wa Afrika, AU, na kubadilisha muundo wa jumuiya hiyo. Makao makuu ya Umoja wa Afrika yako Addis Abeba nchini Ethiopia licha ya juhudi za Libya kutaka yahamishiwe Sirte, mahala alipozaliwa kiongizi wa nchi hiyo, Muammar Ghadhafi.

Baraza lenye umuhimu mkubwa zaidi ndani ya Umoja wa Afrika ni mkutano wa viongozi wa mataifa. Baraza hilo linaweza kuamua kupitia wingi wa theluthi mbili. Kila mwaka viongozi wote wanamchagua mmojawao kuchukua uwenyekiti wa Umoja wa Afrika. Mkutano wa mawaziri wa masuala ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika unathibiti maamuzi yaliyokubaliwa yatekelezwe.

Bunge la Afrika nzima limeanzishwa mwaka 2004 na pia linakutana Addis Abeba. Kila bunge la taifa linatuma wawakilishi watano. Lakini bunge hilo kwa sasa linaweza kutoa ushauri tu. Ili kuwa na Shirikisho la mataifa ya Kiafrika ingebidi bunge hilo liweze kupitisha sheria.

Sehemu kubwa ya kazi ndani ya Umoja huu zinafanywa na baraza la Umoja wa Afrika linaloundwa na komisheni mbalimbali zinazoshughulikia masuala maalum. Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ni tangu miaka minne iliyopita ni aliyekuwa rais wa Mali, Alpha Oumar Konaré. Baraza la Usalama wa Umoja wa Afrika ambalo ni chini ya halmashauri ya Umoja huu lina jukumu na kuchukua hatua kuzuia au kusimamisha vita, uhalifu dhidi ya binadamu au mauaji ya kimbari. Mara ya kwanza Umoja wa Afrika umetuma jeshi katika nchi moja mwanachama, yaani Burundi, mnamo mwaka 2003. Wanajeshi pia wametumwa Darfur lakini jeshi hilo limeshindwa kuleta amani. Sasa kuna mpango huko kuwa na jeshi la pamoja la Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

Hilo pia linazungumziwa kuhusu mzozo wa Somalia ambapo hadi sasa kuna wanajeshi wa kutoka Uganda tu; nchi nyingine zilizoahidi kutuma wanajeshi hazijatimiza ahadi zao. Kwa hivyo, kwa ujumla, lengo la Umoja huu kuitatua yenyewe mizozo barani Afrika bado halikufikiwa.