1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiMalaysia

Miaka kumi toka kutoweka kwa ndege MH370 ya Malaysia

Saleh Mwanamilongo
8 Machi 2024

Muongo mmoja uliopita mnamo Machi 8, Ndege ya shirika la ndege la Malaysia Airlines ilitoweka na haijulikani mahali ilipo, nhilo ni moja kati ya mafumbo makubwa zaidi ya ajali za ndege duniani.

https://p.dw.com/p/4dJeD
Wachunguzi bado hawajui ni nini hasa kilichotokea kwa ndege hiyo pamoja na abiria wake 239
Wachunguzi bado hawajui ni nini hasa kilichotokea kwa ndege hiyo pamoja na abiria wake 239Picha: Arif Kartono/AFP

Miaka kumi baada ya mama yake kutoweka kwenye ndege MH370 ya shirika la ndege la Malaysia, Grace Nathan bado anasumbuka juu ya kukubali kwamba hayupo. Grace alikuwa na umri wa miaka 26 na mwananfunzi wa chuo kikuu wakati ndege iliyowabeba watu 239 ilipotoweka kwenye skrini za rada mnamo Machi 8, mwaka 2014, baada ya kupaa kutoka Kuala Lumpur kuelekea Beijing, China.

Licha ya msako mkubwa zaidi katika historia ya usafiri wa anga, ambao ulihusisha kilomita za mraba 120,000 za sakafu ya bahari ya kusini mwa Bahari ya Hindi, ni vipande vichache tu vya ndege ya Boeing 777-200 vilivyopatikana. Grace kutoka Malaysia amesema kila mwaka unaopita ndege haipatikani na ni mwaka mwingine wa kusubiri.

''Tunahitaji kuwaona kama wako hai''

Mtoto wa Liu Shuang Fong mwenye umri wa miaka 28 Li Yan Lin alikuwa akirejea Beijing kwa sababu wazazi wake walitaka kumtambulisha kwa bibi-arusi mtarajiwa, bahati mbaya hakuwahi kukutana naye. Liu amesema toka tukio hilo, aliamua na mkewe kuhama nyumba yao kwenda mahali papya ili kuondoa hisia zao.

''Maombi yetu ni kutaka kujua ukweli, ndege hiyo na watu waliokuwemo ndani yake wako wapi. Tunahitaji kuwaona kama wako hai. La sivyo tunahitaji kuiona miili yao kama walikufa.", alisema Liu.

Kwa upande wake, Jacquita Gonzales, ambaye mume wake alikuwa mhudumu katika ndege hiyo, amesema njia pekee ya kutatua huzuni yao ni kutafuta ndege hiyo.Kwa waathiriwa wengine, maumivu yaliyohisiwa katika muongo mmoja uliopita ni mara nyingi zaidi kuliko huzuni yao ya awali.

Msako wa MH370 kuanza tena

Miaka kumi baadae familia zinaendelea kusubiri majibu ya kitendawili hicho
Miaka kumi baadae familia zinaendelea kusubiri majibu ya kitendawili hichoPicha: Arif Kartono/AFP

Wiki hii, Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim alisema yuko tayari kufungua tena utafutaji wa ndege hiyo ikiwa ushahidi wakutosha utaibuka. Wakati huo huo, jamaa za abiria na wahudumu wa ndege hiyo ya MH370 wanakabiliana na kutokuwa na uhakika wa kile kilichotokea kwa wapendwa wao.

Waziri wa Uchukuzi wa Malaysia Anthony Loke amesema atakutana na maafisa wa kampuni ya uchunguzi wa baharini yenye makao yake makuu nchini Marekani ya Ocean Infinity kujadili uwezekano wa kuanza tena msako huo.

Kutoweka kwa ndege hiyo kwa muda mrefu kumekuwa mada ya nadharia nyingi za kuaminika hadi potofu. Ripoti ya mkasa huo iliyotolewa na Malaysia mwaka wa 2018 ilionyesha kufeli kwa huduma ya udhibiti wa anga na kusema mwendo wa ndege ulibadilishwa ghafla kwa mikono, lakini ripoti hiyo haikutoa hitimisho lolote thabiti.