1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba mpya wa Umoja wa Ulaya

P.Martin17 Oktoba 2007

Kabla ya kufanywa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya hii leo mjini Lisbon,Rais wa Kamisheni ya umoja huo,Jose Manuel Barroso ametoa mwito kwa viongozi kuwa tayari kuafikiana.

https://p.dw.com/p/C7hG

Mkutano huo unalenga kuondosha shaka za Poland na Italia kuhusu marekebisho ya Mkataba wa Umoja wa Ulaya.

Viongozi wa serikali na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya katika mikutano yao siku ya Alkhamisi na Ijumaa watajaribu kuafikiana na kuondosha tofauti za maoni,ili waweze kuwa na msimamo mmoja kuhusu mkataba mpya wa Umoja wa Ulaya.Mkataba huo mpya uliofanyiwa marekebisho unatazamiwa kuchukua nafasi ya Katiba iliyoshindwa kuidhinishwa.

Ikiwa safari hii,wanachama hao 27 watashindwa kuafikiana,basi uaminifu na uwezo wa kujadiliana wa Umoja wa Ulaya utatiwa mashakani.Kwa sababu hiyo,Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kabla ya mkutano huo wa kilele alieleza hivi:

„Ni dhahiri kuwa tutajitahidi tuwezavyo kupata makubaliano ili mkataba huo uweze kutiwa saini rasmi katika mwezi wa Desemba.“

Hata Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso alisisitiza:

“Hakuna sababu ya kutoafikiana kuhusu mkataba uliofanyiwa marekebisho marekebisho ya mkataba.”

Mkataba huo unatazamiwa kurahisisha utaratibu wa kupitisha maamuzi kwa njia ya kidemokrasia katika umoja uliopanuka ukiwa na wanachama 27 hivi sasa. Vile vile utaimarisha zaidi Bunge la Ulaya na uwakilishaji wa umma wa madola hayo.

Suala lililozusha mvutano mkubwa kuhusu mkataba huo mpya ni ugawaji wa kura katika Umoja wa Ulaya.Juni iliyopita mjini Brussels,kiongozi wa Poland,Jaroslaw Kaczynski hakutaka kukubali kuwa Poland isiyo na hata nusu ya idadi ya wakaazi nchini Ujerumani,itakuwa na kura chache kulinganishwa na Ujerumani.Warsaw ilingangania kuwa rasmi kiwepo kifungu maalum kuhusu upigaji kura,kitakachoweza kutumiwa na mataifa madogo kujadili upya maamuzi yaliyopitishwa kwa uwingi.

Lakini sasa,serikali ya Poland ina matatizo mengine nyumbani,kwani siku mbili baada ya mkutano wa Lisbon,nchini Poland kunafanywa uchaguzi.Na uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni,unaonyesha kuwa chama cha Kazcynski kipo nyuma kabisa kulinganishwa na vyama vikuu vya upinzani.

Raia wengi wa Poland hawakufurahishwa na msimamo mkali uliochukuliwa na serikali yao.Kwa hivyo hivi karibuni hata Rais Lech Kaczynski alie pacha wa Jaroslaw alipunguza ukali wa maneno yake.