1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20 kuijadili Ugiriki na madeni ya eneo la euro

4 Novemba 2011

Ajenda katika mkutano wa mataifa 20 yenye viwanda imegubikwa zaidi na suala la mzozo wa madeni katika eneo la umoja wa sarafu ya euro , pamoja na mtafaruku wa kisiasa nchini Ugiriki.

https://p.dw.com/p/134rx
Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou akiwasili katika kikao cha dharura cha baraza lake la mawaziri.Picha: dapd

Ajenda katika mkutano wa mataifa 20 yenye viwanda imegubikwa na suala la mzozo wa madeni wa mataifa ya eneo la euro pamoja na mtafaruku wa kisiasa nchini Ugiriki. Akizungumza na waandishi habari baada ya mkutano na mwenyeji wa mkutano huo , rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy, rais wa Marekani Barack Obama amesisitiza haja ya kutatua mzozo wa madeni wa ulaya haraka. Rais Sarkozy amesema kuwa sarafu ya pamoja na eneo la euro inapaswa kulindwa kwa gharama zote. Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble , ambaye amekuwa akikutana na wenzake mjini Cannes, amedai kuwa Ugiriki itoe jibu la wazi kuhusiana na iwapo inataka kubakia katika sarafu ya euro. Schäuble amekiambia kituo cha taifa cha televisheni ya Ujerumani kuwa ni sawa tu iwapo jibu litapatikana kutokana na kura ya maoni ama uchaguzi wa ghafla. Suala kuu , amesema , ni kwamba Ugiriki inapaswa kuamua iwapo ina ridhia na ina uwezo wa kutekeleza hatua ilizokubali ili kuweza kupata fungu la pili la fedha za uokozi.