1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya

Hamidou, Oumilkher10 Juni 2008

Rais Bush ahudhuria mkutano wake wa mwisho wa kilele pamoja na umoja wa ulaya

https://p.dw.com/p/EGrT
Rais Bush na waziri mkuu wa Slovenia Janez JansaPicha: AP


Miezi kama saba hivi kabla ya kumaliza mhula wake katika ikulu ya Marekani-White House,rais George W. Bush anatazamiwa kuhudhuria mkutano wa mwisho wa kilele kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya hii leo, akilenga kuwatanabahisha washirika wake wakubali kuishinikiza zaidi Iran iachane na mradi wake wa kinuklia.


Rais George W. Bush aliyewasili jana usiku Ljubljana amepangiwa kukutana na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya José Manuel Barroso pamoja na waziri mkuu wa Slovenia Janez Jansa,mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya,kabla ya kufika ziarani nchini Ujerumani,Ufaransa,Italy na baadae nchini Uingereza.


Washington na serikali za nchi za Umoja wa Ulaya hazifikirii kama taarifa kali kali zitatolewa mnamo wakati huu wa kumalizika utawala wa rais Bush uliogubikwa na upinzani mkali wa nchi kadhaa za Ulaya dhidi ya vita nchini Irak.

Kwa mujibu wa mswaada wa taarifa ya mwisho ya mkutano huo wa kilele,iliyolifikia shirika la habari la Reuters,Marekani na Umoja wa Ulaya wanasema wako tayari kutangaza vikwazo ziada vya Umoja wa mataifa dhidi ya Iran ikiwa Teheran itaendelea kupuuza madai ya kusitisha shughuli zake za kinuklea.


Baadhi ya wanadiplomasia wa magharibi waliashiria hivi karibuni utayarifu wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya,wa kupindukia vikwazo vya Umoja wa mataifa.Wanazungumzia uwezekano wa kuzuwiliwa milki na kutangazwa marufuku ya kusafiri baadhi ya viongozi wa serikali ya Iran.


Rais George w. Bush aliyekua akikosolewa barani Ulaya kwa kile kinachotajwa kua "diplomasia ya kimabavu",anajitahidi kuregeza kamba kuelekea washirika wake wa Ulaya.


Naibu mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya Günther Verheugen alisema hivi karibuni:


"Ushirikiano wetu ni wa dhati na wa bidii.Unatulazimisha sisi wa kutoka Ulaya tuwajibike zaidi katika majukwaa ya kimataifa,lakini unawalazimisha pia marafiki zetu wa Marekani watilie maanani ukweli kwamba jukumu la kuiongoza dunia si la mmoja."


Mbali na Iran, suala la mabadiliko ya hali ya hewa nalo pia litajadiliwa katika mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani.


Mwenyekiti wa baraza la Umoja wa Ulaya,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Slovenia Dimitrij Rupel amesema licha ya hitilafu za maoni zilizopo katika suala la ulinzi wa hali ya hewa kuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano kuhusu waraka wa pamoja kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya.



►◄