1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika mjini Lisbonne

Oummilkheir7 Desemba 2007

Umoja wa Ulaya wasaka ushirika wa dhati na wa haki pamoja na nchi za Afrika

https://p.dw.com/p/CYsD
Picha: picture-alliance / dpa

Miaka sabaa baada ya mkutano wao wa kwanza wa kilele mjini Cairo,viongozi wa Umoja wa ulaya na Afrika wanakutana mjini Lisbonne,wakitaraji kutia njiani uhusiano sawia katika wakati huu ambao bara la Afrika linazidi kuyavutia mataifa makuu ya Asia na hasa China.

Zaidi ya viongozi 70 wa taifa na serikali wanahudhuria tukio hilo la kidiplomasia ambalo halijawahi kushuhudiwa nchini Ureno.

Viongozi wamenza kuwasili tangu alkhamisi mjini Lisbonne,ikiwa ni pamoja na rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, japo kama mkutano wenyewe wa kilele unaanza leo jumamosi.

Uengereza inawakilishwa na waziri wa zamani bibi Valerie Amos pamoja na malodi,baada ya waziri mkuu Godron Brown kukataa kuketi meza moja pamoja na rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anaelaumiwa kwa kuziendeya kinyume haki za binaadam.

Hata hivyo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uengereza David Miliband amesema nchi yake iko tayari kuchangia katika ushirika wa nguvu kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika na akuisaidia Zimbabwe pia ikiwa na hapa tunanukuu “uhuru utaheshimiwa nchini humo.”Mwisho wa kumnukuu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uengereza David Miliband.

Mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya,waziri mkuu wa ureno José Socrates,mkutano huu wa pili wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika unabidi uanzishe “sio tuu mkakati wa ulaya kuelekea Afrika,bali pia ubuni mkakati wa pamoja,na kwa mara ya kwanza katika historia.

“Tunabidi tugeuze ukurtasa wa historia ya baada ya ukoloni na kuanzisha ushirikiano wa kweli utakaotuwama katika misingi ya usawa kati ya Ulaya na Afrika.”amesisitiza kwa upande wake katibu wa dolas wa ureno anaeshughulikia masuala ya ushirikiano Joao Gomes Cravinho.

Suala la Zimbabwe,hata kama halimo katika ajenda ya mazungumzo,huenda likazungumziwa kwa namna moja au nyengine na baadhi ya viongozi wa umoja wa Ulaya.

Mwenyeji wa mkutano huu wa kilele,waziri mkuu wa Ureno José Socrates anasema:

“Mada kuhusu uongozi jumla wa serikali,mazingira,mabadiliko ya hali ya hewa,namna ya kukabiliana na wimbi la wahamiaji na pia tutazungumzia masuala ya haki za binaadam…Yote hayo yameorodheshwa katika mkakati wa pamoja.”

Umoja wa ulaya na Umoja wa Afrika wameorodhesha mada kuhusu pia amani na usalama,demokrasia na haki za binaadam,biashara na maendeleo,nishati na uhamiaji na ajira.

Mkakati wa pamoja unatazamiwa kupitishwa jumapili ijayo na viongozi wa taifa na serikali,pamoja na mpango wa vitendo utakaofafanua mada nane za ushirikiano wa dhati unaobidi kutekelöezwa katika kipinmdi cha miaka mitatu ijayo,kabla ya mkutano ujao wa kilele ambao kimsingi unatakiwa ufanyike mwaka 2010 barani Afrika.

Maandamano kadhaa yamepangwa kufanyika pembezoni mwa mkutano huu wa kilele kulalamika dhidi ya kuhudhuria Mugabe mkutanoni na dhidi ya kutokuwepo mjadala kuhusu Darfour.

Askari polisi elfu tatu na askari wa gendarmerie wamewekwa kusimamia usalama wakati wa mkutano huo wa kilele unaofanyika katika jingo kubwa lililoko mashariki ya Lisbone pamoja pia na hoteli 22 waliokofikia washiriki wa mkutano huo wa kilele.