1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Bara Afrika na Umoja wa Ulaya wamalizika

P.Martin10 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CZWS
Kansela wa Ujerumani,Angela Merkel amemkosoa Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe kuhusu ukiukaji wa haki za binadamuPicha: AP

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Afrika umemalizika mji mkuu wa Ureno,Lisbon kwa kutiwa saini mkakati mpya wa ushirikiano.Huo ni mkutano wa pili kufanywa na pande hizo mbili,tangu ule wa mwaka 2000 mjini Cairo,Misri.

Kwa sehemu kubwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika,ulifanywa faraghani. Mara kwa mara waandishi wa habari waalipewa taarifa fupi.Ni viongozi wachache tu waliochukua muda kutoa maelezo kwa urefu kama vile Waziri Mkuu wa Uhispania Jose Luis Zapatero,Rais wa Senegal,Abdoulay Wade na Waziri Mkuu wa Cape Verde,Jose Maria Neves.

Sehemu kubwa ya majadiliano ya wanasiasa hao yalifanywa nyuma ya milango iliyofungwa. Yasikitisha,kwani mkutano wa Lisbon ungekuwa nafasi nzuri ya kujadili wazi wazi hali mbaya ya haki za binadamu katika nchi nyingi za Kiafrika na kuutia moyo umma.Kwani orodha ni ndefu….kwa mfano Darfur,Zimbabwe,Somalia,Angola, Eritrea na kadhalika.

Hata hivyo,mkutano wa Lisbon kinyume na hofu za wengi,haukutenga kabisa suala la haki za binadamu.Kwani ukingoni mwa mkutano huo wa kilele,viongozi wa Ulaya walimueleza Rais wa Sudan Omar al-Bashiri kuwa Sudan inapaswa kujitahadi zaidi kuviunga mkono vikosi vya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.Na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel,alisema wazi wazi kuwa hali ya haki za binadamu nchini Zimbabwe haikubaliki.

Hayo ni maendeleo kulinganishwa na ule mkutano wa miaka saba iliyopita mjini Cairo.Hata hivyo ingekuwa bora zaidi kama majadiliano hayo yangefanywa hadharani.Kwani ni nadra kwa Ulaya kupata nafasi kama hiyo kuueleza umma wa Afrika msimamo wa Ulaya kuhusu haki za binadamu, demokrasia na utawala wa kisheria.

Hasi ni kuwa viongozi wa Ulaya walijaribu kutenga majadiliano kuhusu mkataba mpya wa biashara huru, unaojulikana kama Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiiuchumi-EPA.Lakini baadhi ya nchi za Kiafrika zilitumia nafasi ya mkutano wa Lisbon kueleza kinagaubaga kuwa hazikubaliani ni vile Ulaya inavyoendesha majadiliano ya kibiashara.Rais wa Senegal,Abdoulaye Wade alikwenda umbali wa kusema kuwa Mkataba wa Kiuchumi umekufa na kutoa mwito wa kuanzishwa majadiliano mapya kabisa.Hilo ni pigo kwa wajumbe wa Umoja wa Ulaya ambao hadi dakika ya mwisho walikuwa na matumaini. Wamestahili kupata pigo hilo kwani wajumbe wa Ulaya walijaribu kupitia mlango wa nyuma kujadili mada ya mkataba wa biashara huria kama vile huduma za masoko ya Afrika,licha ya kuwa kuambatana na Shirika la Biashara Duniani WTO hizo si mada za kujadiliwa tena.

Tofauti hizo za maoni ni sehemu ya ushirikiano kati ya washirika sawa.Na kila upande unapaswa kuvumilia:Ulaya kuhusu mkataba wa kiuchumi na Afrika kuhusu mada ya demokrasia na haki za binadamu.