1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa chakula Roma mwezi ujao

4 Oktoba 2009

Kitisho cha njaa na utapia mlo chazidi kuongezeka.

https://p.dw.com/p/JxRc
FAO, World Food Summit, Logo, Italien, Rom, http://www.fao.org/worldfoodsummit/english/index.html

Mkutano wa kilele wa viongozi wa dunia kuhusu usalama wa chakula unatarajiwa kufanyika mjini Roma tarehe 16 hadi 18 mwezi ujao wa Novemba , huku wataalamu wakionya kwamba hali ya usalama wa chakula duniani imezidi kuwa mbaya na kuzidisha pia kitisho kwa uhai wa binaadamu. Kwa mujibu wa makadirio ya hivi karibuni ya Umoja wa mataifa, idadi ya watu duniani itaongezeka kutoka bilioni 6.8 hadi bilioni 9.1 ifikapo 2050. Theluthi moja zaidi ya binaadamu watakaohitaji chakula.

Kinachokatisha tamaa:

Bei za juu za chakula katika nchi hiyo, msukosuko wa kiuchumi duniani utakaoathiri ajira, kuongezeka kwa umasikini na idadi kubwa zaidi ya wenye njaa ni mambo ambayo ukiyachanganya, yanatoa sura ya kukatisha tamaa.Kwa hiyo nini matumaini ya mashirika matatu ya chakula ya Umoja wa mataifa yalioko mjini Roma ? Kiongozi wa idara ya uchumi wa maendeleo ya kilimo katika Shirika la chakula na kilimo la umoja wa mataifa lenye makao yake makuu katika mji huo mkuu wa Italia, Kostas Stamoulis anasema mkutano mkuu ujao hautokua wa kuchangisha fedha kwani msimamo wa awali ulikua ni kumaliza njaa ifikapo 2025, ingawa anasisitiza kwamba hana uhakika kama hilo litakua ndiyo lengo la mkutano huo mkuu, kwa sababu nchi wanachama bado hazijakubaliana juu ya mkakati wa kuchukuliwa na kwamba Utaratibu huo unapaswa kuratibiwa vizuri zaidi, kwa sababu hadi sasa kila msukosuko hugeuka kuwa janga.

Ongezeko la Idadi ya watu :

Ongezeko kubwa la idadi hiyo ya watu duniani litakua katika nchi zinazoendelea.Pamoja na hayo licha ya utajiri uliopo duniani lakini kumeshuhudiwa pia hali ya kuongezeka kwa watu wenye njaa duniani kwa idadi kubwa kuwahi kuonekana tangu 1996.Ripoti ya karibuni ya Shirika la kilimo na chakula la umoja wa mataifa FAO,inasema kwa kuzalisha asili mia 70 zaidi ya chakula kwa nyongeza ya watu ya 2.3 bilioni ifikapo 2050, wakati huo huo ukipigwa vita umasikini na njaa kwa kutumiwa mali asili zilizo adimu vizuri zaidi na kwenda sambamba na badiliko la hali ya hewa, ni changamoto kubwa itakayoikabili sekta ya kilimo duniani katika miongo ijayo.

kilicho muhimu:

Kilicho muhimu hivi sasa ni kuhakikisha wakulima wanasaidiwa na kupewa motisha sio tu katika nchi zilizoendelea bali pia katika nchi zinazoendelea. Katika mkutano wa kilele wa kundi la nchi manane tajiri G8 uliofanyika Julai mjini L`Aquila Italia, viongozi wa nchi hizo waliamua kuchangisha dola bilioni 20 katika miaka mitatu ijayo kupambana na msukosuko wa chakula na ikasemekana fedha hizo zitatumiwa kuinua kilimo kuliko kuwa ni msaada. Hata hivyo baadhi ya wadadisi wana shaka shaka juu ya hilo na badala yake wanasema kinachohitajika ni kubadilishwa kwa mfumo mzima wa kile kinachozusha hali hiyo ya msukosuko wa chakula duniani, ikiwa ni pamoja na kuboreshwa mfumo wa utoaji onyo na mapema na uratibu bora zaidi.

Majukumu ya mashirika husika:

Wenyeji wa mkutano ujao FAO ni moja wapo ya mashirika matatu ya umoja wa mataifa yenye makao makuu mjini Roma kila moja likiwa na malengo tafauti. FAO ni jukwaa ambamo mataifa yote hukutana kujadiliana juu ya mikataba na sera.Fuko la kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo IFAD lina jukumu la kugharimia miradi ya maendeleo vijijini .Na Shirika la mpango wa chakula duniani WFP hukusanya misaada ya chakula kutoka mataifa ya viwanda na kusambaza kwa wenye mahitaji ya chakula katika nchi zinazoendelea.

Kwa mujibu wa takwimu za 2008 na 2009, idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa na utapia mlo duniani imeongezeka kwa milioni 100. Hiyo ni moja wapo ya changamoto ya Viongozi watakaokutana Novemba mjini Roma.

Mwandishi:M.Abdul-Rahman/IPS

Mhariri:Martin,Prema