1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Umoja wa ulaya mjini Brussels

Hamidou, Oumilkher14 Machi 2008

Viongozi wa umoja wa ulaya wamekubaliana juu ya kuundwa umoja wa nchi za mediterenia

https://p.dw.com/p/DOVL
Kansela Angela Merkel akizungumza na waandishi habari mjini BrusselsPicha: AP


 Umoja wa ulaya unapanga kutathmini upya siasa yake kuelekea nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia.Hayo yameamuliwa katika mkutano wa viongozi wa umoja huo mjini Brussels.


Viongozi wa taifa na serikali wa umoja wa ulaya wamekubaliana katika mkutano wao mjini Brussels,kuunga mkono pendekezo la Ufaransa na Ujerumani kuhusu Umoja wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia,utakaozijumuisha nchi zote 27 wanachama wa umoja wa ulaya.Kwa namna hiyo viongozi wa umoja wa ulaya wameunga mkono msimamo wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliyepinga hapo awali fikra iliyotolewa na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ya kubuni kilabu ya nchi zinazopakana na bahari ya kati.


Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy alisema baadae "amevutiwa na jinsi kansela Angela Merkel alivyoutetea mpango huo wa kuundwa Umoja wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia.


Kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy walifikia makubaliano tangu mapema mwezi huu,ya mpango huo ambao baadhi ya viongozi walikua na hofu nao hapo awali.


 Tangu zaidi ya miaka kumi iliyopita Umoja wa ulaya umetia njiani kile kijulikanacho kama "utaratibu wa Barcelona"ambao lengo lake ni kuwa na uhusiano wa dhati zaidi pamoja na nchi zinazopakana na bahari ya kati mfano Algeria na Moroko.Mpango huo lakini umekwama kwasababu ya mvutano kati ya nchi za kiarabu zinazopakana na bahari hiyo ya kati na Israel.


Wajumbe mkutanoni wanashuku kama kubadilishwa jina na kuitwa Umoja wa nchi za bahari ya mediterenia kutabadilisha chochote.Makubaliano ya kuanzishwa umoja huo yatatiwa saini July 13 ijayo mjini Paris,Ufaransa itakapokua mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa ulaya kwa nusu ya pili ya mwaka huu wa 2008.


Hitilafu za maoni zinakutikana katika malengo yaliyowekwa mwaka mmoja uliopita ya hifadhi ya hali ya hewa.Hapo kansela Angela Merkel hakufanikiwa kuushawishi msimamo wake  uungwe mkono na wote mkutanoni.Kansela Angela Merkel alipendelea kuona viongozi wa umoja wa ulaya wanakubaliana juu ya tarehe ya kutiwa njiani kanuni maalum kwaajili ya viwanda vya chuma pua na viwanda vya saruji.Kansela Angela Merkel amesema:


"Mijadala kuhusu viwanda vinavyotumia nishati kwa wingi na kwa mitindo mmoja inahusu suala kama mwaka 2009 ndipo tutakapotamka jinsi shughuli za kibiashara zitakavyokua baada ya mwaka 2012,ili wateja waweze kutambua kinachowasubiri,au kama tusubiri kwanza mwaka 2010 ,halafu ndio tuamue jinsi itakavyokua.Kwa hivyo suala hapa si kiwango cha kuhifadhiwa hali ya hewa,nionavyo mie hili ni suala la kimsingi na la busara ili kuwapatia hakikisho wateja, vitega uchumi vyao vitahifadhiwa."


Msimu wa kiangazi mwaka 2007 Ujerumani ilipokua mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya,viongozi wa umoja huo walikubaliana moshi wa viwandani upunguzwe kwa asili mia 20 hadi ifikapo mwaka 2020.


Viongozi wa Umoja wa Ulaya wametia saini kwa mara ya kwanza waraka unaozungumzia madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa kwa usalama wa Ulaya.Wakimbizi walioyapa kisogo maskani yao kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa,uhaba wa maji na ukosefu wa mafuta na gesi ni miongoni mwa mambo yaliyodhukuriwa ndani ya waraka huo.




►◄