1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mataifa ya umoja wa Ulaya na Asia kuanza leo.

Kitojo, Sekione23 Oktoba 2008

Viongozi wa mataifa 45 ya Asia na Ulaya wanakutana leo katika mkutano wao wa siku mbili katika mji mkuu wa China , Beijing.

https://p.dw.com/p/FfTG

Viongozi wa mataifa 45 ya Asia na Ulaya wanakutana kuanzia leo tarehe 24 hadi 25 mwezi Oktoba katika mji mkuu wa China Beijing. Mkutano huo kati ya mataifa ya ulaya na yale ya Asia mwaka huu unafanyika kwa kauli mbiu inayosema mwelekeo na hatua za kivitendo, kuelekea suluhisho litakaloridhisha kila upande.

Katika mazungumzo hayo mkutano huo unalenga katika kupanua na kuimarisha majadiliano kati ya Ulaya na Asia na utendaji wa pamoja katika uchumi.

Mkutano huo wa viongozi wa mataifa ya Ulaya na Asia , ASEM ni jukwaa lisilokuwa rasmi la majadiliano kati ya mataifa hayo. Kila baada ya miaka miwili makundi hayo ya mataifa hukutana ili kubadilishana mawazo kuhusu mada na matatizo baina ya mataifa ya Asia na umoja wa Ulaya.

Wazo la kuanzishwa jukwaa hilo la ushirikiano limetokana na waziri mkuu wa zamani wa Singapore, Goh Chok Tong. Katika mwaka 1994 waziri mkuu wa zamani wa Ufaransa Edouard Balladur alisisitiza haja ya kuwa na jukwaa kama hilo na kuimarisha uhusiano baina ya mataifa ya Ulaya na Asia.

Mashauriano ya kwanza yalifanyika March 1996 mjini Bangkok, ambapo lilianzishwa rasmi jukwaa la ASEM.

Tangu wakati huo kundi hilo lilipanuliwa mara mbili. Kundi kubwa kabisa linaloshiriki mkutano huo ni mataifa 27 ya umoja wa Ulaya na tume ya umoja wa Ulaya , mataifa 10 wanachama wa umoja wa mataifa ya Asia ASEAN , ikiwa ni pamoja na Brunei, Indonesia, Kambondia , Laos, Malaysia , Mynamar, Philippines, Singapore, Thailand na Vietnam. Nyingine ni China , Japan , Korea ya kusini, India, Pakistan na Mongolia.

Leo hii mataifa hayo wanachama wa ASEM wanawakilisha zaidi ya nusu ya watu wote duniani. Kwa pamoja wanachangia kiasi cha asilimia 60 ya uchumi wa dunia pamoja na asilimia 50 ya mapato jumla ya biashara ya dunia.

Ndio sababu rais wa kamisheni ya umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso akayahimiza mataifa makubwa ya kiuchumi barani Asia jana , kama Japan , China na India kuwa yanapaswa kuchukua jukumu la kupambana na mzozo wa kifedha duniani. Barroso amewaambia waandishi wa habari kabla ya mkutano huo kuanza leo , kuwa dunia inapaswa kujifunza somo hili la mzozo wa kifedha ili kuweza kufanyia mageuzi mfumo wa kifedha duniani.

Tunalihitaji bara la Asia kuhusika , amesema, na kuongeza kuwa ushiriki wa China, India na Japan ni muhimu kwa ajili ya kupata ufumbuzi katika mzozo huu.

Hali inayoongezeka ya utegemezi katika uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa ya Asia na Ulaya , kutafakari sera za kiusalama, na mapambano dhidi ya ugaidi ni masuala ambayo yatakuwa mbele katika ajenda za mkutano huo wa ASEM, kama yalivyo masuala ya uhamiaji, mabadiliko ya hali ya hewa na ulinzi wa mazingira.

Utendaji wa pamoja baina ya mataifa ya Asia na Ulaya tangu mwanzo haukukosa hali ya wasi wasi na matatizo. Mataifa ya umoja wa Ulaya mara kwa mara yanakumbana na ushindani mkubwa hata hivyo kuweza kuingia katika soko la mataifa ya Asia.


►◄