1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Ukimwi Vienna.

20 Julai 2010

Matumaini makuu kwa wanawake kufuatia uvumbuzi wa malham ya kukinga virusi vya ukimwi.

https://p.dw.com/p/OPqH
Mkutano wa 18 wa kimataifa wa ukimwi Vienna.Picha: AP

Mkutano wa 18 wa kimataifa  unaojadili masuala ya Ukimwi umeingia siku yake  ya tatu huko mjini Vienna,Austria.Baada ya mivutano kuhusu masuala ya ufadhili na gharama ya kutoa huduma za dawa za kupambana  na makali ya Ukimwi,taarifa  njema zimejitokeza katika kikao  hicho.Wanasayansi walitangaza kuwa utafiti mpya umebaini  kwamba matumizi ya malham maalum yanasaidia katika mapambano dhidi ya maambukizi  ya  virusi   vya HIV.Malham  hiyo tayari imefanyiwa majaribio Afrika Kusini  na huenda ikawa njia moja muhimi ya kuwakinga  wanawake ambao wanaubeba mzigo mkubwa zaidi wa ugonjwa Ukimwi.

Malham hiyo iliyofanyiwa uchunguzi Afrika kusini, inazuia hatari ya maambukizi ya virusi hivyo vya ukimwi,  kwa asilimia 39, lakini kwa kwa wale wanawake walioitumia mfululizo,iliupunguza uwezekano huo kwa asilimia 54.

Malham hiyo ina asilimia 1 ya kemikali aina ya tenofovir ambayo ni mojawapo ya kemikali zinazopatikana katika madawa ya kupunguza makali ya ugonjwa huo, ARV's,inayoipunguza kasi ya kuongezeka virusi vya  HIV mwilini mwa binaadamu.

Utafiti huo uliotangazwa katika mkutano unaoendelea wa 18 wa kimataifa wa ukimwi mjini Vienna, umepokelewa kwa shangwe na wanaharakati wa masuala   ya ukimwi duniani.Hata hivyo wanasayansi walitahadharisha kuwa majaribio zaidi yanahitajika kwani  kwa sasa  yamefikia kwenye  awamu ya pili.Kulingana  na majaribio hayo malham hiyo maalum inaweza kuipunguza kasi ya virusi vya HIV  kuongezeka mwilini na pia haina athari zozote.

Hatahivyo wanasayansi hao wamesema hii inaleta matumaini, maana bila ya malham hiyo katika muda wa mwaka wanawake 10 wanaambukizwa virusi vya ugonjwa huo, huku kutokana na matumizi wake, idadi hiyo inapungua hadi wanawake 6.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la umoja wa mataifa la UNAIDS,Michel Sidiba, alisema utafiti huu unawapa wanawake matumaini na kwa mara ya kwanza wametoa nafasi kwa wanawake kuamua wenyewe, na kujikinga na virusi vya ugonjwa huo.

Michel ameongeza kuwa iwapo itadhibitishwa, malham hiyo itakua ndio njia ilio na nguvu na itasiadia kukabiliana na janga la ugonjwa huo hatari.

Mkuu wa shirika la afya duniani WHO,Margaret Chan, aliahidi kuwa shirika hilo la Umoja wa mataifa litajitahidi kikazi kuharakisha upatikanaji wa dawa hiyo punde tu itakapo dhibitishwa kuwa salama kwa utumitzi na inafanya kazi.Utafiti huo uliochapishwa na jarida la Marekani,Science,ulipangwa kuwa ajenda ya kuzungumziwa katika warsha ya hapo kesho jumatano itakayokuwa siku ya tatu ya mkutano huo wa kimataifa wa ukimwi.

Iwapo itaidhinishwa, basi malham hiyo itajiunga na dawa zinazoongezeka za kinga dhidi ya virusi hivyo vya ukimwi.

Watu milioni 25 wameuwawa na ugonjwa hatari wa ukimwi mpaka hivi leo, huku zaidi ya milioni 33 wameambukizwa  virusi vinavyosababisha ugonjwa huo.

Zaidi ya thuluthi mbili ya idadi hizi,  ni watu wanaoishi katika eneo la Afrika lililo kusini mwa jangwa la Sahara ambapo asilimia 60 ya maambukizi mapya hutokea kwa wanawake na wasichana.

Njia mojawapo kubwa inayozidisha kusambaa kwa ugonjwa huu ni kupitia kufanya mapenzi na waathirika wanaokaidi kuvaa kondom.

Mwandishi:Maryam Abdalla/AFPE

Mhariri:Mwadzaya,Thelma