1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri S.Gabriel afungua mkutano

Mtullya, Abdu Said19 Mei 2008

Mkutano wa nne wa Umoja wa Mataifa juu ya kulinda viumbe na mazingira yaliyomo katika hatari ya kutoeka umefunguliwa leo mjini Bonn na waziri wa mazingira wa Ujerumani bwana Sigmar Gabriel.

https://p.dw.com/p/E2Qj
Waziri wa mazingira wa Ujerumani Sigmar Gabriel akifungua mkutano juu ya ulinzi wa mazingira mjini Bonn .Picha: AP

Waziri  wa ulinzi  wa mazingira wa Ujerumani bwana  Sigmar Gabriel ametoa  mwito kwa jumuiya ya kimataifa  juu ya  kuchukua  hatua  za haraka  ili kuepusha  kuteketezwa viumbe na  mazingira. Waziri Gabriel amesema dunia sasa  imefikia mahala pabaya  ambapo  mazingira  na  mimea ya aina mbalimbali  inatoeka kwa haraka.

Waziri Gabriel  amesema hayo katika hotuba yake ya kufungua  mkutano  juu ya kulinda viumbe na mazingira yalimo hatarini  kutoeka unaofanyika mjini Bonn nchini  Ujerumani.

Mkutano  huo wa siku tisa unahudhuriwa na  wajumbe  wapatao 6000 kutoka nchi 190.

Katika juhudi  za kupambana na hatari ya mazingira na viumbe vya aina mbalimbali  kutokomea kansela wa Ujerumani Angela Merkel  anatarajiwa kutangaza nyongeza ya fedha kwa  ajili ya kusaidia juhudi  hizo.

Mkutano  huo  wa nne unaofanyika chini ya udhamini wa Umoja  wa Mataifa na uenyekiti wa Ujerumani unajadili njia za ufanisi za kupambana na hatari zinazotishia maeneo kama misitu muhimu na viumbe mbalimbali duniani.