1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUhispania

Mkuu wa shirikisho la soka Uhispania akataa kujiuzulu

25 Agosti 2023

Mkuu wa shirikisho la soka la Uhispania Luis Rubiales amekataa kujiuzulu baada ya kumbusu mdomoni nyota wa Kombe la Dunia la Wanawake Jenni Hermoso kufuatia ushindi wa Uhispania wa Kombe la Dunia la FIFA.

https://p.dw.com/p/4Vaqw
Mkuu wa Shirikisho la Kandanda la Uhispania Luis Rubiales akimbusu Jenni Hermoso wa timu ya taifa ya wanawake ya Uhispania
Mkuu wa Shirikisho la Kandanda la Uhispania Luis Rubiales akimbusu Jenni Hermoso wa timu ya taifa ya wanawake ya UhispaniaPicha: Chris Putnam/ZUMA Wire/IMAGO

Hatua yake ilizua hasira miongoni mwa wachezaji na mawaziri wa serikali walioshutumu tabia hiyo na kuitaja kama isiyokubalika.

Akizungumza katika mkutano wa dharura wa shirikisho la soka la Uhispania RFEF, Rubiales amelalamika kwamba "wanaharakati wa uwongo wa wanawake” walikuwa wanajaribu kumuua.

Ameelezea tukio hilo kama "busu dogo” ambalo lilifanyika haraka, kwa msisimko kutokana na furaha, hiari na kwa makubaliano.

"Je, busu la hiari litanitoa hapa? Sitojiuzulu. Nitapigana hadi mwisho,” Rubiales amesema na kushangiliwa na wafuasi ambao wengi wao walikuwa ni wanaume.

Ukosoaji juu ya tabia ya Rubiales umeendelea kwa wiki sasa. Tukio hilo lilitokea wakati wachezaji walipokuwa wakikabidhiwa medali zao baada ya Uhispania kuifunga England 1-0 katika fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake mjini Sydney, Australia mnamo siku ya Jumapili.

Soma pia: FIFA kufungua kesi dhidi ya rais wa shirikisho la soka la Uhispania 

Wakati wachezaji walipokuwa jukwaani, Rubiales alimbusu mdomoni Jenni Hermoso.

Serikali imethibitisha leo kuwa italiwasilisha tukio hilo mbele ya mahakama ya michezo, ambapo iwapo litathibitishwa kuwa lisilofaa kimaadili, huenda Mkuu huyo wa shirikisho la soka la Uhispania akashtakiwa chini ya sheria ya unyanyasaji wa kijinsia iliyoanzishwa na chama tawala cha Kisosholosti mwaka uliopita.

Hotuba ya Rubiales katika mkutano wa shirikisho la soka la Uhispania RFEF, imeibua ukosoaji kutoka kwa kaimu Waziri wa leba Yolanda Diaz, aliyeitaja kama "isiyokubalika.”

"Serikali lazima ichukue hatua za haraka, kutoadhibiwa kwa vitendo vya kutojali au kutoonyesha hisia umekwisha. Rubiales hafai kuendelea kusalia ofisini,” Diaz ameandika kwenye mtandao wa kijamii.