1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU: Mwanajeshi wa Uganda auwawa

1 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCDT

Mwanajeshi wa Uganda ameuwawa kwenye mapigano yanayoendelea mjini Mogadishu nchini Somalia. Kifo cha mwanajeshi huyo ni cha kwanza cha wanajeshi wa Umoja wa Afrika wanaolinda amani nchini Somalia.

Msemaji wa jeshi la Uganda, meja Felix Kulaije, amesema wanajeshi wa Uganda walikuwa wakiilinda ikulu ya rais wa serikali ya mpito ya Somalia hapo jana wakati waliposhambuliwa na maroketi ambapo mwanajeshi huyo aliuwawa.

Mapigano mjini Mogadishu yameingia siku yake ya nne hii leo huku wanamgambo wa kiislamu wakiendelea kukabiliana na majeshi ya serikali ya mpito ya Somalia yakisaidiwa na majeshi ya Ethiopia.

Wakaazi wanaoishi karibu na uwanja mkubwa wa kandanda mjini Mogadishu wamesema mabomu yameanza kuvurumishwa kutoka eneo la kusini mwa mji mkuu huo kuanzia mwendo wa saa tatu unusu leo asubuhi hivyo kuzusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia.

Shirika la msalaba mwekundu limeyaeleza mapigano ya mjini Mogadishu kuwa mabaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha zaidi ya miaka 15.

Majeshi ya serikali yanasema yamewaua wafuasi zaidi ya 200 wa viongozi wa mahakama za kiislamu waliofurushwa kutoka Mogadishu mwishoni mwa mwaka jana.

Raia wengi wamejeruhiwa katika mapigano hayo na inaripotiwa hospitali zimejaa majeruhi. Maelfu ya Wasomali wanaukimbia mji wa Mogadishu katika juhudi za kuyasalimisha maisha yao.