1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU: Wanajeshi zaidi wa Ethiopia waingia Somalia

2 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCDC

Mamia ya wananajeshi wa Ethiopia wameingia mjini Mogadishu nchini Somalia hii leo baada ya siku nne za mapigano makali yaliyosababishwa na operesheni ya jeshi la Ethiopia dhidi ya wanamgambo wa kiislamu na wapiganaji wa kimbari.

Wakaazi wa Mogadishu wanasema wanajeshi hao wameingia mjini humo kupitia barabara inayotokea mjini Baidoa makao makuu ya serikali ya mpito ya Somalia.

Majeshi ya Ethiopia yanashika doria katika kitongoji cha Ali Kamin karibu na uwanja mkubwa wa kandanda, ambako mapambano makali yamekuwa yakiendelea na ambako kumesikika milio ya risasi mapema leo.

Balozi wa Marekani nchini Kenya, Michael Ranneberger, amesema Marekani ina wasiwasi juu ya machafuko ya Somalia na akazitaka pande husika zirejee katika meza ya mazungumzo.

´Bila shaka Marekani ina wasiwasi mkubwa juu ya kiwango cha machafuko yanayoendelea hasa ikizingatiwa kwamba raia wengi wasio na hatia wanaumia. Tunawahimiza wote wanaohusika katika mapigano warejee kwenye mdahalo wa maridhiano ya kitaifa. Hiyo ndiyo njia ya pekee itakayoleta usalama na uthabiti nchini Somalia.´

Shirika la wakimbizi la Umoja wa mataifa, UNHCR, limetangaza kwamba Wasomali elfu 47 wameukimbia mji wa Mogadishu katika siku kumi zilizopita.

Huku utulivu ukiwa umerejea tena mjini humo, milio ya risasi imesikika katika eneo la kusini la Area Four.