1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU : Wapiganaji wa Kiislam wajiandaa kwa vita

25 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCpU

Muungano wa mahkama za Kiislam umesema umekuwa ukipeleka maelfu ya wapiganaji na silaha nzito kwenye medani za mapambano leo tayari kwa vita na serikali dhaifu ya mpito nchini Somalia na washirika wao wa Ethiopia.

Uongozi wa mahkama hizo za Kiislam umesema wameimarisha maeneo yalioko nje ya makao makuu ya serikali huko Baidoa kama kilomita 225 kaskazini magharibi mwa Mogadishu wakitarajia kushambuliwa na umeishutumu nchi jirani ya Ethiopia kwa kutuma ndege za kivita.

Akizungumza na shirika la habari la AFP Mkuu wa majeshi wa wanamgambo wa Kiislam Sheikh Muktar Robow amesema wako tayari kabisa kwenye medani hizo na kwamba wamejichimbia kwenye mahandaki yao.Amesema wanakabiliana na wavamizi wa Ethiopia na jambo pekee wanalotarajia ni kuanza kwa mapambano.

Amesema Waethiopia wamepeleka ndege za kivita zikiwemo helikopta na vifaru huko Baidoa na kwamba wanakusudia kuanzisha shambulio dhidi yao.