1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Bunge la Somalia laidhinisha kutumia sheria za kijeshi nchini humo.

13 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCav

Bunge la Somalia limepiga kura kuidhinisha kutumiwa sheria ya kijeshi nchini humo na hivyo kuiruhusu serikali ya mpito kutangaza hali ya hatari itakayoendelea kwa muda wa miezi mitatu.

Naibu Spika wa bunge amesema wabunge mia moja na hamsini na wanne waliunga mkono hatua hiyo na wawili wakaipinga.

Sheria hiyo imepitishwa punde baada ya taarifa kutolewa kwamba majeshi ya serikali hiyo, yanayosaidiwa na Ethiopia, yaliteka ngome ya mwisho ya wanamgambo wa Kiislamu kusini mwa nchi hiyo.

Msemaji wa serikali alisema majeshi yamekiteka kijiji cha pwani cha Ras Kamboni ambako wanamgambo wa Kiislamu walikuwa wamekimbilia.

Taarifa zinasema wanamgambo wengi wamekamatwa.