1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Jeshi la Ethiopia lakubaliana na Jamii ya Hawiye

23 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCGJ

Jeshi la Ethiopia limefikia makubaliano ya kusitisha mapigano na jamii ya Hawiye ya Wasomali iliyo na ushawishi mkubwa mjini Mogadishu.Hayo ni kwa mujibu wa viongozi wa jamii hiyo.Makubaliano hayo yanatokea siku moja baada ya serikali kusisitiza kuwa itaendelea na mapigano mpaka wanamgambo wa kiislamu watakaposhindwa nguvu.Wengi wa wapiganaji hao ni wa jamii ya Hawiye na wanalaumiwa kuhusika na mashambulizi kadhaa mjini humo.

Kulingana na msemaji wa jamii hiyo Ugas Abdi Dahir Mohammed ,jamii hiyo imekubaliana na jeshi la Ethiopia kusitisha vita baada ya mazungumzo.Makubaliano hayo aidha yanawahusisha majeshi ya serikali ya muda ya Somalia wanaotegemea ushirikiano wa jeshi la Ethiopia lilo na vifaa.

Hali inaripotiwa kuwa shwari hii leo mjini Mogadishu baada ya mapigano ya siku mbili yaliyosababisha vifo vya watu 24 na kujeruhi wengine kadhaa.

Maafisa wa kijeshi wa Ethiopia wanathibitisha kuwa mkutano kuhusu makubaliano hayo ulifanyika kwenye nyumba ya Abdi Hassan Qeybid,mbabe mmoja wa kivita.Hata hivyo hawakuthibitisha iwapo makubaliano ya kusitisha vita yamefikiwa.Hii ni mara ya kwanza kwa makubaliano ya aina hiyo kufikiwa kwa mujibu wa jamii hiyo ya Hawiye.Somalia imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 91 baada ya Rais Siad Barre kungolewa madarakani.