1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto wa bomba la mafuta wachoma watu 100 mjini Lagos

Kalyango Siraj16 Mei 2008

Wengi wawaliokufa walikuwa watoto wa shule iliokuwa karibu

https://p.dw.com/p/E1DA
Mama huyu analia baada ya bomba la mafuta kulipuka na kushika moto na kuwauwa watu 260 mjini Disemba 26 mwaka 2006.Karibu miaka mitatu baadae tukio lingine kama hilo limetokea mjini Lagos katika mtaa wa Ijegun alhamisi 16.05.08 ambapo watu 100 wameuawa, wengi wao wakiwa watoto wa shule.Picha: AP

Takriban watu 100 wameuawa katika mlipuko uliotokea katika bomba la mafuta katika mji wa Lagos nchini Nigeria.

Mashahidi wanasema watu 50 walikufa papo hapo.Wazima moto nao wanapambana siku ya pili mfululizo ili kuweza kuuzima.

Idadi ya waliopoteza maisha yao katika moto wa mjini Lagos,kwa mujibu wa maofisa wa chama cha msalaba mwekundu, wanafikia 100,na wengi wao ni watoto.Kwani mlipuko katika bomba la mafuta uliosababisha moto huo, ulitokea karibu na shule katika mji wa kibiashara wa Lagos.

Wazima moto wamefaulu kuuzima baada ya shirika la mafuta kukata mafuta kupitia bomba hilo lililoharibiwa na tingatinga moja lililokuwa linafanya shughuli mahali hapo.Pia inasemekana mvua ilionyesha ilirahisisha kazi ya wazima moto.

Eneo kuliko tokea mlipuko huo limefungwa.

Moto huo ulianza alhamisi mchana na kuendelea kuwaka usiku kucha huku ukitoa moshi mkubwa .Moto huo ulichoma magari, maduka kadhaa ya karibu katika kiunga cha Ijegun.Pia shule moja iliokuwa karibu nayo ilichomwa na moto huo.

Mwanafunzi mmoja mwenye umri wa miaka 19,amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa,mlipuko ulitokea wakati wakifanya mtihani.Ameendelea kuwa wananchi walisaidia kuvunja ukuta mmoja ili kuwawezesha kutoroka.

Na wazima moto walijaribu kadri ya uwezo wao kuona kama moto huo hausogelei kituo cha kuuzia mafuta kilichokuwa karibu.

Moto unayosababishwa na mabomba ya mafuta hutokea kila mara nchini Nigeria ambayo ni mojawapo wa mataifa ya kiafrika yanayozalisha mafuta kwa wingi.

Wachambuzi wanasema sababu moja inayosababisha moto huo ni ukarabati duni wa mabomba hayo.Pia wezi wa mafuta nao wanachangia sana,wakibomoa mabomba hayo wakitaka kujichotea mafuta na kuyauza kimagendo.

Watu 40 walifariki siku ya Krismasi mwaka jana mjini Lagos baada ya kuchomwa moto uliotokea katika bomba moja ambalo liliharibiwa na wezi wa mafuta.Mwaka mmoja kabla, watu wengine zaidi ya 200 walikufa walipokuwa wanachota mafuta kutoka bomba ambalo liliharibiwa mjini Lagos.

Takriban wanakijiji 1,000 na Ushei walifariki mwaka wa 1998 katika sehemu moja ya eneo lenye mafuta la Niger Delta baada ya bomba moja la mafuta kuharibiwa.

Inafikiriwa wahanga walikuwa wakichota mafuta wakipanga kuyauza kimagendo.

shirika la kitaifa la mafuta la Nigeria NNPC limelalamikia uharibifu wa kila mara unaofanywa dhidi ya mabomba yake ya mafuta.

Shirika linasema kuwa mambomba yake huharibiwa karibu kila mwaka.Visa vya uharibifu hutokea aidha mara 400 ama 500 kwa mwaka.

Kwa mda huohuo,mke wa meneja mmoja wa kampuni ya mafuta ya Ufaransa Total wa ofisi ya mkoa wenye mafuta unaopatika kusini mwa Nigeria wa Rivers, ametekwa nyara na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha.

Hakujatolewa habari za kutaka fidia ili kuachiliwa huru mwanamke huyo alietekwa jana karibu na nyumba yake mjini Port Harcourt.

Katika kipindi cha miaka miwili iliopita kumekuwa na visa vya utekaji nyara vikifanywa na majambazi ambayo hudai fidia.Laiki pia kuna utekaji nyara mwingine ambao unahusiana na masuala ya siasa.