1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshauri wa zamani wa rais Kibaki aikosoa serikali kwa rushwa

Charo Josephat /RTRE10 Februari 2009

Rushwa ndicho kitu kinachoishikilia serikali ya umoja wa kitaifa

https://p.dw.com/p/GqlX
Waziri mkuu Raila Odinga, (kushoto) na rais Mwai KibakiPicha: AP

Ufisadi ndicho kitu kinachoishikilia serikali ya umoja wa kitaifa nchini Kenya. Hayo yamesemwa na bwana John Githongo, mshauri wa zamani wa rais wa Kenya Mwai Kibaki kuhusu vita vya kupambana na rushwa nchini humo. Lakini waziri wa mashauri ya kigeni wa Kenya bwana Moses Wetangula anasema serikali bado inaendelea na juhudi zake za kupambana na rushwa.

Rais Mwai Kibaki na waziri mkuu Raila Odinga walilazimika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi wa Desemba 2008 ili kukomesha mauaji yaliyokuwa yakiendelea kufuatia matokeo ya uchaguzi huo yaliyozusha utata. Lakini wadadisi wanasema serikali ya viongozi hao imeshindwa kuangamiza vitendo vya rushwa nchini Kenya.

Bwana John Githongo, aliyekuwa zamani mshauri wa rais Mwai Kibaki katika maswala ya kupambana na rushwa amesema sasa imedhihirika wazi kwamba serikali ya Kibaki na waziri mkuu Odinga inaendelea kuwepo kwa sababu ya rushwa na wala sio mpango wowote wa kuleta mageuzi wala maadili ya pamoja.

Akijibu madai hayo ya Githongo, waziri wa mashauri ya kigeni wa Kenya, Moses Wetangula, amesema si ya kweli na kwamba bwana Githongo hajui kinachoendelea kwa kuwa haishi Kenya bali huingia na kutoka.

Bi Gladwell Otieno wa taasisi ya Afrika ya utawala wa uwazi mjini Nairobi, anasema Kenya kwa sasa inakabiliwa na matatizo mengi na mazito ya rushwa. Aidha bi Otieno amesema serikali imepuuza majukumu yake muhimu ya kuleta neema kwa Wakenya wengi wanaokabiliwa na balaa la njaa na umaskini, badala yake viongozi wanapiga mbio kujinufaisha wenyewe.

''Inaonekana maslahi makubwa ya serikali hii ni kuhakikisha inaendelea kuwepo huku kila mbunge akijaza tumbo lake. Wanapata marupurupu mengi na wameungana katika lengo la kujitajirisha. Kuna mzozo mkubwa sana wa ufisadi kwa wakati huu nchini Kenya.''

Kenya inakabiliwa na upungufu mkubwa wa mahindi, chakula kinacholiwa kote nchini humo baada ya mahindi yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye maghala ya kitaifa kuisha. Baadhi ya wabunge wamemtaka waziri wa kilimo William Ruto, ambaye ni mshirika mkubwa wa waziri mkuu Raila Odinga, ajiuzulu mara moja ili kuruhusu uchunguzi ufanyike. Ruto amepuuziliambali wito huo.

Habari zilijitokeza ni kuwa baadhi ya wabunge walinunua kiwango kikubwa cha mahindi kutoka ghala la kitaifa la nafaka, hatua inayosemekana ilichangia kusababisha upungufu mkubwa wa mahindi nchini.

Akizungumzia swala la mahindi waziri Wetangula amesema kuna tume inayochunguza swala hilo na atakayepatikana na hatia atabeba msalaba wake.

Visa vya rushwa nchini Kenya vinawakatisha tamaa Wakenya wa tabaka la chini waliopiga kura kutaka mabadiliko yatakayowasaidia kuboresha maisha yao.

Bi Gladwell Otieno wa taasisi ya Afrika ya utawala wa uwazi ameitaka jumuiya ya kiraia nchini Kenya kujizatiti kuwahamasisha Wakenya, kuwapa changamoto wanasiasa katika maeneo yao na kuwaongoza watu waliochoshwa na tabia ya wabunge kukataa kulipa kodi, kuishinikiza serikali itekeleze wajibu wake.