1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa vyama vya Wasunni watishia kutoka serikalini

P.Martin8 Novemba 2006

Machafuko yakiendelea nchini Irak,chama kikuu cha Wasunni bungeni hii leo kimetishia kuachana na utaratibu wa kisiasa na kitashika silaha ikiwa serikali inayodhibitiwa na Washia itaendelea kupuza wito wa kuwanyanganya silaha wanamgambo.

https://p.dw.com/p/CHLD

Msemaji wa muungano wa vyama vitatu vya Kisunni vilivyo na viti 44 bungeni,bwana Salim Abdallah amesema,kundi hilo lilituma waraka kwa serikali majuma mawili ya nyuma kuitaka ichukue hatua ya kuwanyanganya silaha wanamgambo.Amesema,ikiwa serikali haitotekeleza ombi hilo basi huenda wakajitoa kwenye utaratibu wa kisiasa na hawatokuwa na njia nyingine isipokuwa kushika silaha.Tangazo hilo limetolewa,baada ya serikali ya waziri mkuu Nuri al-Maliki inayodhibitiwa na Washia kukosolewa vikali hiyo jana na makamu wa rais,Tareq al-Hashemi alie Msunni,kwamba Wairaki hawatendewi haki sawa.Akizungumza mji mkuu wa Qatar-Doha,bwana al-Hashemi amesema,serikali haikutimiza ahadi zilizotolewa kwa vyama vya Kisunni hasa juu ya suala la kuendeleza usawa kati ya makundi mbali mbali.

Mwezi wa Mei,al-Maliki aliunda serikali ya umoja iliyojumuisha vyama vya kisiasa na makundi mbali mbali kwa azma ya kufikiria mahitaji ya jamii tofauti nchini Irak.Serikali hiyo lakini inadhibitiwa na al-Maliki na muungano wake wa Washia.Wasunni wanaituhumu serikali ya al-Maliki kuwa inazidi kupendelea maslahi ya Washia na inapuuza harakati za wanamgambo wa Kishia, ikidaiwa kuwa wao ndio wanaohusika na mauaji ya Wasunni.Desemba mwaka 2005,Wasunni waliposhiriki katika uchaguzi,hatua hiyo ilichukuliwa kama ni ushindi mkubwa katika utaratibu wa kuleta umoja na amani nchini Irak.Lakini mwanya kati ya jumuiya hizo mbili umezidi kuwa mkubwa,huku mauaji ya kimadhehebu yakiendelea pamoja na shutuma za upendeleo katika vikosi vya usalama vinavyodhibitiwa na Washia.

Mmuagiko wa damu ukizidi nchini Irak,watu 7 waliuawa mapema leo asubuhi,katika mashambulio yaliorejea katika eneo la mji mkuu Baghdad baada ya amri ya kuzuia watu kutoka nje kuondoshwa.Amri hiyo ilitangazwa wakati wa kutolewa adhabu ya kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Saddam Hussein. Kufuatia kutangazwa kwa adhabu ya kunyongwa ya Saddam Hussein,maandamano ya kuunga mkono na kupinga adhabu hiyo yalifanywa sehemu mbali mbali nchini Irak.

Wimbi la machafuko likiendelea nchini humo,leo hii jeshi la Marekani limearifu kuwa mwanajeshi wake mmoja amefariki kutokana na majeraha aliopata wakati wa mapigano yaliozuka kwenye wilaya ya Anbar.Idadi ya wanajeshi wa Kimarekani waliouawa nchini Irak mwezi huu sasa imefikia 20.Ripoti zinasema,tangu vita vya Irak kuanza mwezi wa Machi mwaka 2003,si chini ya wanajeshi 2,838 wa Marekani wameuawa nchini humo.