1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa fedha na madhara yake

Hamidou, Oumilkher16 Oktoba 2008

Viongozi wameingia mbioni kuunusuru uchumi wa dunia

https://p.dw.com/p/FbB5
Kishindo katika soko la hisa la Frankfurt nchini UjerumaniPicha: AP



Hofu na wasi wasi mkubwa umetanda katika masoko ya hisa ya dunia hii leo baada ya kuporomoka hisa katika masoko ya mjini Tokyo na New-York katika wakati ambapo barani Ulaya sauti zinaanza kupazwa kutaka pawepo "taasisi mpya ya Bretton Woods",kuufanyia marekebisho mfumo wa fedha ulimwenguni.


Baada ya kuporomoka kwa asili mia 11.4 mjini Tokyo,na asili mia 7.87 mjini New-York,masoko ya hisa barani Ulaya yanajiandaa kukabiliana na misuko suko mengine hii leo:Masoko ya hisa mijini London,Paris na Frankfurt,kila moja limepoteza zaidi ya asili mia 5,robo saa tuu baada ya kufunguliwa hii leo.


Masoko mengine ya hisa barani Asia yamekumbwa na mkosi sawa na huo yalipokua yanafungwa hii leo.Seoul imepoteza asili mia 9.4,Syndney asili mia 6.7 na Shanghai asili mia 4.25.Katika nchi za Ghuba pia masoko ya hisa yameporomoka,tukichukua mfabno wa lile la Dubai lililopoteza zaidi ya asili mia 6.


Mbali na mzozo wa fedha kuna hofu zilizozuka uchumi wa dunia pia huenda ukaporomoka.


Mjini Brussels,mnamo siku ya pili ya mkutano wao wa kilele,viongozi wa Umoja wa ulaya wanatazamiwa kutoa mwito wa kufanyiwa marekebisho ya kina mfumo wa fedha wa dunia,kabla ya mkutano pamoja na rais George W. Bush,jumamosi ijayo huko Camp David Marekani.


Mjini New-Delhi,viongozi wa Brazil,India na Afrika kusini wamezituhumu nchi tajiri kusababisha mzozo huu.


Kiongozi wa Cuba,Fidel Castro amezikaripia "nchi za kibepari za ulaya" akihoji haziko katika hali ya kulazimisha masharti na ufumbuzi wao kwa ulimwengu uliosalia.


Viongozi wa Ulaya wanataka,miongoni mwa mengineyo,ziondolewe nafuu za kodi za mapato katika baadhi ya nchi na mashirika ya walanguzi.


Viongozi wa mijini London na Berlin wanashauri pia lifanyiwe marekebisho shirika la fedha la kimataifa kuweza kutwaa jukumu la kusimamia shughuli za kiuchumi ulimwenguni.


Akizungumzia haja ya kufanyiwa marekebisho taasisi za fedha za kimataifa,kansela Angela Merkel amesema.


Ndio maana naunga mkono moja kwa moja fikra ya kuitishwa mkutano wa viongozi wa taifa na serikali,kabla ya mwaka huu kumalizika,pengine mwezi ujao wa November,Viongozi wa mataifa muhimu ya G8 na mataifa tajiri kiviwanda watakutana na viongozi wa mataifa yanayoinukia kutafakari juu ya mfumo mpya wa fedha ulimwenguni na mapendekezo yatolewe kuhakikisha hali hii haitokei tena..."


Nchi za Ulaya zinailaumu Marekani kubeba sehemu ya dhamana ya mzozo huu wa fedha,kutokana na kukataa kwake kwa miaka kadhaa,shughuli katika masioko ya fedha zisikaguliwe sana.


Mzozo wa fedha umeisibu pia Uswisi.Serikali ya mjini Zurich na benki kuu ya Uswisi zimesema,zitachangia faranga bilioni sita za Uswisi katika hazina ya benki ya UBS na kudhamini hisa za hadi dala bilioni 60 za benki hiyo.


Crédit Suisse,benki ya pili kubwa nchini Uswisi imetangaza nyongeza ya raslimali yake kwa faranga bilioni 10 za Uswisi,katika wakati ambapo taasisi hiyo imekula hasara ya faranga bilioni moja nukta tatu mnamo robo ya tatu ya mwaka huu.


Ishara mojawapo ya ughali wa mafuta ni ile hali kwamba bei ya mafuta ghafi imeendelea kuporomoka hii leo,pipa moja limeuzwa chini ya dala 68,ikilinganishwa na dala 147 mwezi July uliopita.