1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Gaza

Eric Kalume Ponda2 Februari 2009

Israel imefanya mashambulio mapya ya angani katika eneo la ukanda wa Gaza ambako Mpaletsina mmoja yaripotiwa kuuawa.

https://p.dw.com/p/GlqE
Zana za jeshi la Israel. Je wanajeshi wa Israel wanarudi Gaza?Picha: AP

Shambulio hilo limetekelezwa kujibu mashambulio la awali la mizinga 10 ya maroketi yaliyovurumishwa mapema katika eneo la Kusini mwa Israel na kuwajeruhi watu 3 wakiwemo wanajeshi wawili. Kwa upande mwengine mashauriano ya kutafuta amani yaliendelea mjini Cairo Misri huku mivutano ikijitokeza katika pande zote mbili kwenye mzozo huo.


Rais Mahmud Abbas ambaye alikua na mazungumzo na mwenyekiti wa mpango wa amani wa mashariki ya kati rais Hosni Mubaraka wa Misri, alionya kuwa makundi yanayopingana na chama cha Hamas katika eneo la Gaza, yanatishia usalama wa Wapalestina na mpango huo wa amani kwa jumla.


Rais Abbas alisema haya baada ya mashauriano hayo yaliyochukua muda wa masaa mawili na pia kuhudhuriwa na waziri wa mambo ya nje wa Saudia mfalme Saud al- Faisal. Itakumbukwa kwamba Saudi Arabia ni mshirika muhimu katika mpango huo wa amani.

Chama cha Hamas hata hivyo kinasisitiza kuwa hakihusika na mashambulio hayo ambayo yamekuwa yakiendelea tangu kusimamishwa kwa vita hivyo tarehe 18 mwezi uliopita.

Jumla ya makombora 10 ya maroketi yalishambulia eneo la kusini mwa Israel, na kusababisha Israel kujibu kwa kufanya mashambulio makali ya anga katika eneo la Gaza ambako Mpalestina mmoja aliuawa na wengine 4 wamejeruhiwa.


Kadhalika Wanajeshi wa Israel walimuua Mpalestina mmoja katika eneo la ukingo wa magharibi,baada ya Mpalestina huyo kuwafyatulia risasi wanajeshi wa Israel waliokuwa wakishika dora.


Hata hivyo kuna mgawanyiko miongoni mwa viongozi wa Israel kuhusu iwapo Israel iendeleze mashambulio ndani ya Gaza au la.


Waziri wa Ulinzi Ehud Baraka amesema kuwa suala hilo bado halijaidhinishwa na baraza la usalama nchini Israel,na hivyo kutofautiana na msimamo wa waziri wa mambo ya nchi za nje Tzipi Livni anayesisitiza kuwa Israel haitasita kufanya mashambulio ndani ya Gaza na haipasi kutambua chama cha Hamas.


Tofauti hizo zinaonekana machoni mwa wengi kuwa kampeni ya Barak wa chama cha Leba na Livni wa chama cha Kadima ambao ni wagombea wakuu kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 10 mwezi huu.


Huku hayo yakiendelea wajumbe wa chama cha Hamas wanaohudhuria mashauriano hayo mjini Cairo wametangaza huenda wakakubali kwa masharti kutia saini mkataba wa kusimamisha mapigano kwa muda wa mwaka mmoja.


Masharti hayo ni kufunguliwa kwa vituo vyote vya mpakani kikiwemo cha mji wa Rafah na kuondoka kabisa kwa Israel ndani ya Gaza.

Hata hivyo hatua hiyo itategemea mshikamano wa makundi yanayopingana katika ukanda wa Gaza miongoni mwayo kundi la Fatah linalooongozwa na rais Mahmud Abbas.


Kiongozi wa chama cha Hamas anayeishi uhamishoni nchini Lebanon Khaled Meshaal amekipuuza chama kikuu cha ukombozi wa Wapalestina PLO chini ya uongozi wa rais Mahmud Abbas akisema kimepoteza umaarufu wake. Rais Abbas amesisitiza kuwa hakuna mashauriano yatakafanyika na Hamas bila ya kutambua PLO.


Habazi zaidi zinarifu kuwa rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy ambaye kwa ushirikiano na rais HosnI Muabarak walifanikisha mpango wa kusimamisha kwa muda mashambulio mwezi uliopita, amekua na mazungumzo na mjumbe wa rais Barack Obama George Mitchell ambaye amekamilisha ziara yake katika eneo la mashariki ya kati kutoa msukumo zaidi wa kufikiwa amani ya kudumu katika eneo hilo. Pia rais Sarkozy anatarajiwa kukutana na Rais Mohamud Abbas baadaye hii leo.


Ponda/Afp-Reuters