1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa gesi kati ya Urusi na Belarus

23 Juni 2010

Mvutano kuhusu masuala ya gesi na malipo kati ya Urusi na Belarus umechukua sura mpya hii leo baada ya kampuni ya Gazprom ya Urusi kukipunguza kiasi cha gesi inayoifikia Belarus kwa asilimia 30.

https://p.dw.com/p/O0iK
Nembo ya kampuni ya nishati ya GazpromPicha: picture-alliance/dpa

 Kiasi hicho  ni sawa na  punguzo la  asilimia 60 ya matumizi  yote ya siku. Hali  hiyo imesababishwa na deni  la kiasi cha dola milioni 192  la malipo  ya  mafuta ya Belarus.Kwa upande wake Belarus inashikilia kuwa inaidai kampuni  ya nishati ya Urusi ,Gazprom kiasi cha dola milioni 200 kama malipo  ya kusafirishia gesi hadi mataifa mengine ya Ulaya. Katika mkutano na maafisa  wa ngazi za juu, mkurugenzi mkuu wa kampuni ya nishati ya  Urusi ya Gazprom,Alexei  Miller aliitangaza hatua hiyo ya kuipunguzia  kiasi cha gesi kinachoifikia Belarus.Hata hivyo bado kiasi  cha gesi inayosafirishwa kupitia Belarus bado  hakijabadilika wakati  yote hayo yakiendelea.

Punguzo  maradufu

Hapo  jana,Urusi iliamua  kuipunguzia Belarus maradufu  kiasi cha gesi inayoihitaji  kwa siku.Mwanzoni mwa wiki hii  punguzo hilo lilikuwa asilimia 15.Mkurugenzi wa kampuni  ya nishati ya Urusi,Gazprom  Alexei  Miller anasisitiza  kuwa Belarus  kamwe haijachukua hatua zozote za kulilipa deni inalodaiwa.

Urusi  imeonya kuwa punguzo hilo litaendelea sanjari na deni hilo ambalo kwa  sasa linaripotiwa kuwa kiasi cha dola milioni 192.Deni hilo limelimbika tangu mwanzoni  mwa mwaka huu hadi mwezi wa Aprili.Endapo  Urusi italiongeza deni la mwezi  wa Mei  kiasi hicho huenda kikafikia dola  milioni 250.  

Weißrussland Gazprom Energiewirtschaft Russland Deutschland BASF
Wafanyakazi katika kiwanda cha Gazprom,kilicho karibu na mji wa Nesvizh,Belarus.Picha: AP

Wakati huohuo kulingana na maafisa wa serikali  ya  Belarus,mataifa ya eneo la Ulaya ya Magharibi  bado yanaendelea kupata gesi inayotokea  Urusi bila ya matatizo yoyote hata baada  ya Rais Alexander Lukashenko kutishia hapo jana kuisimamisha shughuli hiyo.Kwa  mujibu  wa taarifa ya  serikali ya Belarus,kampuni  yake ya kusafirishia gesi ya Beltransgaz , imeamriwa kuhakikisha kuwa mfumo wake mzima unafanya kazi bila ya  vikwazo  vyovyote  kwa minajili ya kuyakimu  mahitaji ya wateja wake.Mkurugenzi wa Shirika la  Gazprom Alexei Miller  alisema  kuwa'',Tunajitahidi  kufanya kila tuwezalo ilikuhakikisha kuwa wateja wetu wa bara la Ulaya hawaathiriki kwa njia yoyote ile.''alieleza.

Wanadaiana?

Hapo jana  Jumanne,maafisa  wa serikali  za Belarus  na Urusi walilijadili suala la madeni wanayodaiana.Rais Lukashenko alilirejelea tena  ombi  lake la kuongezewa muda  wa  kuzitafuta  dola milioni 192 inazodaiwa na  Urusi.Belarus inadai  kuwa tayari imeshailipa  Urusi kiasi kisichojulikana  cha matumizi ya   mwezi  wa Mei.Wakati huohuo Belarus inadai kwamba Urusi haijailipa kiasi cha dola milioni 260  kama malipo ya kusafirishia gesi kwa kipindi  cha miezi mitano ya mwanzo wa  mwaka huu. 

Huku  mzozo huo ukiendelea,mataifa hayo  mawili  yametangaza kuwa ushirikiano kati yao katika  suala   la nishati  umeimarika.Kwa mujibu  wa Waziri  wa nishati  wa Urusi Sergei Shmatko aliyezungumza na shirika  la  habari  la ITAR-Tass,nchi yake inajiandaa kuzuwia  matatizo  yoyote kuwafikia wateja wake wa mataifa  ya  Ulaya magharibi.Hatua  hizo zinajumuisha  kuwa na waangalizi wasioegemea  upande wowote wakati  wa usafirishaji pamoja na mauzo ya gesi. 

 Awali mivutano  ya   gesi  kati  ya  Urusi  na Ukraine  iliyasababisha mataifa ya Ulaya  kutokuwa na bidhaa hiyo muhimu hususan katika msimu wa baridi.Kwa  upande  wake  Umoja wa Ulaya umeuondoa wasiwasi huo kwa  kiasi  cha asilimia 6.25  ya gesi yote inayohitajika barani  Ulaya inatokea Belarus.Msemaji wa Idara ya mambo ya  nje katika Kamisheni  ya Umoja wa  Ulaya Marlene Holzner ,''Hatuna taarifa  zozote zinazoeleza kuwa huduma za gesi zimesitishwa katika taifa la Lithuania.Endapo hilo limetokea basi basi  kama tulivyosema  Latvia itaisafirishia gesi hiyo kwakiopindi cha wiki moja.Kwa  sasa,hatuwezi  kujua kitakachotokea baada ya wiki  hii ,''amelieleza hilo.

Gazprom Bau der Ostsee-Pipeline beginnt
Kisima cha mafuta bahariniPicha: AP

Chachu ya mvutano

 Ifahamike kuwa  mataifa ya Lithuania,Poland na Ujerumani yanaitegemea gesi  ya Urusi inayosafirishwa kupitia Belarus. 

 Kulingana  na vyombo vya habari vya Urusi,mvutano  huo umesababishwa  na Belarus inayoipinga  hatua yake  ya kuanzisha ushurikiano wa  forodha  itakayoijumuisha  pia Kazakhstan.Waziri wa mambo  ya nje  wa Belarus,Sergei  Martynov,anaripotiwa kueleza kuwa nchi yake inataka halmashauri hiyo  kuwapa washirika wote haki sawa.Kiongozi huyo aliyasema hayo hapo jana  Jumanne alipokutana  mjini Minsk na mwenzake  wa  Urusi.Wachambuzi  nao wanaeleza  kuwa mzozo huo unachagizwa na hali  kwamba Belarus inajisogeza karibu zaidi na Umoja wa Ulaya  kinyume na ilivyokuwa awali ikishirikiana kwa karibu zaidi na Urusi.     

Huku  yote  hayo yakiendelea,mazungumzo ya   suluhu  kati ya pande mbili husika yanatarajiwa kuendelea  hii  leo.

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-AFPE/RTRE

Mhariri:Josephat Charo