1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa kisiasa nchini Ukraine

Maja Dreyer3 Aprili 2007

Mzozo ndani ya serikali ya Ukraine umefika kilele kingine leo hii. Licha ya upinzani wa waziri mkuu Yanukowitsh, rais Yushtshenko jana usiku alivunja bunge la Ukraine na kutangaza uchaguzi mpya ufanyike mwezi wa Mei. Maelfu ya waandamaji wamefiki katika mji mkuu Kiev, wakati hali hii tete inazitia wasiwasi nchi za Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/CB4v
Wafuasi wa waziri mkuu Yanukowitsh mjini Kiev
Wafuasi wa waziri mkuu Yanukowitsh mjini KievPicha: AP

Huu ni mzozo mkali zaidi wa kisiasa tangu kufanyika mapinduzi mwaka 2004 yanayojulikana kama mapinduzi ya rangi ya machungwa. Baada ya taarifa ya rais Yushtshenko ambaye alikuwa kiongozi wa mapinduzi haya kulivunja bunge la Ukraine, maelfu ya wafuasi wa waziri mkuu Yanukowitsh walikuja mjini mkuu Kiev kuandamana dhidi ya amri hiyo. Wabunge wa vyama vya serikali ya mseto chini ya waziri mkuu Yanukowitsh walikutana leo bungeni, huku Yanukowitsh akisema serikali iendelee kufanya kazi kama kawaida hadi mahakama ya katiba itakapoamua juu ya hatua hiyo ya rais Yushtshenko.

Waziri mkuu Yanukowitsh alisema pia atafanya kila awezalo kumshawishi rais Yushtshenko kubatilisha amri yake ya kulivunja bunge. Ama sivyo, rais huyu atabeba dhamana kubwa kwa nchi nzima alisema Yanukowitsh na aliongeza kusema: “Maoni yangu ni kwamba ikiwa ni hivyo basi si tu uchaguzi wa bunge ufanyike bali pia lazima kufanya uchaguzi mpya wa rais.”

Kwa mujibu wa spika wa bunge la Ukraine, rais Yushteshenko na waziri mkuu Yanukowith wamepanga kukutana baadaye leo hii kutafuta suluhisho. Kabla ya hapo, rais Yushtenko alibatilisha amri zote zilizopitishwa na bunge baada ya kuvunjwa kwake. Jana usiku bunge hilo kupitia wingi liliivunja kamati ya uchaguzi na kuzuia fedha za kugharama uchaguzi mpya ambao rais Jushtshenko alisema utafanyika terehe 27 Mei.

Wakati hali mjini Kiew inazidi kuwa tete – maelfu ya waandamanaji walipiga mahema yao karibu na bunge – rais Yushtshenko alitoa mwito kwa jeshi la Ukraine kutoingilia kati katika mzozo huu akisisitiza huo ni mvutano wa kisiasa ambao unafaa kutatuliwa kwa njia ya kisiasa.

Umoja wa Ulaya umearifu una wasiwasi juu ya mzozo huu mpya. Ujerumani ambaye ni mwenyekiti wa Umoja huu, umeitaka Ukraine fuate sheria za katiba na za kidemokrasi. Inabidi pande zote ziwe za utulivu na ziwe tayari kukubaliana. Urusi pia imeelezea wasiwasi wake.

Konstantin Kosatshew, mwenyekiti wa kamati ya masuala ya nchi za nje ya bunge la Urusi, anaikosoa hatua ya rais Yushtshenko: “Hadi hapo hatuoni kuwa chama chochote cha bunge au kundi lolote jingine la kisiasa limevunja katiba. Kwa hivyo rais Yushtshenko hakuwa na sababu yoyote kujiingiza vikali hivyo kwa kulivunja bunge.”

Katika miezi kadhaa iliyopita mvutano kati ya serikali ya mseto chini ya waziri mkuu Yanukowitsh anayesemekana anaungwa mkono na Urusi na upande wa mapinduzi ya rangi ya machungwa ulizidi kuwa mkali. Wabunge wengi wa vyama vya mapinduzi waligeukia kwenye vyama tawala na hivyo kubadilisha mgawayiko wa utawala. Kuna madai kuwa wabunge hawa walipewa rushwa kuvigeuka vyama vyao. Ikiwa wabunge wengine wangebadilisha upande, vyama vya kikomunisti, kisoshialisti na vyama vya kitaifa vinavyoiunga mkono Urusi vingeweza kubadilisha katiba na hivyo kuathiri mamlaka ya rais. Inasemekana kuwa rais Yushtshenko kwa kulivunja bunge anajaribu kuzuia asiathirike.