1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Nuklia wa Iran wazidi kufuka moshi

22 Machi 2007

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linajaribu kufikia makubaliano kuhusu hatua ya kuiwekea vikwazo Iran.

https://p.dw.com/p/CHHh
Rais Mahmoud AhmedNejad asema mradi wa Nuclear utaendelea
Rais Mahmoud AhmedNejad asema mradi wa Nuclear utaendeleaPicha: AP

Wajumbe wanakutana tena leo kutafakari marekebisho ya vikwazo hivyo baada ya Iran kuzionya nchi zenye nguvu kwamba itatetea haki yake ya kuwa na nishati ya Nuklia.

Nchi tano za kudumu kwenye baraza la usalama la Umoja wa mataifa zinajaribu kutia msukumo katika kupatikana mwafaka juu ya azimio la kuiwekea viwazo Iran lakini hadi sasa zimeshindwa kuwashawishi wanachama wengine kwenye baraza hilo kuunga mkono azimio hilo.

Nchi hizo tano zinataka kuzidisha vikwazo vya sasa kwa kupiga marufuku usafirishaji wa silaha kutoka Iran na vile vile kuongeza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya taifa hilo.

Lakini nchi za Afrika Kusini,Indonesia na Qatar zimewasilisha hapo jana mapendekezo ya kufanyika marekebisho katika azimio hilo ambayo yanatajwa huenda yakapunguza makali ya azimio linalojadiliwa kwa sasa.

Baraza la usalama linakutana tena hii leo kujadili marekebisho hayo.

Azimio la sasa linataka Iran ipigwe marufuku kusafirisha silaha, iwekewe vikwazo vya kiuchumi vile vile idadi ya maafisa na makampuni yaliyolengwa kuwekewa vikwazo vya usafiri iongezwe na hivyo kuongeza nguvu vikwazo vilivyowekwa mnamo mwezi Desemba.

Akitetea msimamo wan chi yake kwenye baraza hilo la usalama la umoja wa mataifa juu ya kutaka azimio hilo lirekebishwe Balozi wa Afrika Kusini katika baraza hilo Dumisani Kumalo alikanusha kwamba serikali yake inajaribu kuudhoofisha azimio hilo lililowasilishwa na nchi tano wanachama wa kudumu.

Marekebisho yaliyopendekezwa ni kwamba baraza la usalama lisiwalenge baadhi ya watu binafsi nchini Iran,mabenki na makundi Fulani ambayo hayahusiki na mpango wa Kinuklia wa Iran.

Afrika Kusini imependekeza kwamba Iran ipewe siku 90 badala ya 60 kuzingatia amri ya kuachana na urutubishaji wa madini ya Uranium lakini pendekezo hilo limekataliwa.

Hata hivyo haijaeleweka wazi ni lini azimio hilo litapigiwa kura lakini kwa upande wake

Rais wa Iran Mahmoud AhmedNejad amesema anataka kulihutubia baraza hilo la usalama la umoja wa mataifa juu ya suala hilo kabla kura haijapigwa.

Iran ambayo inaendelea na shughuli zake za urutubishaji wa madini ya Uranium na kukaidi maazimio ya mwanzo ya baraza la usalama imesema haitosimamisha mradi wake wa Kinuklia,

Na badala yake Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema Iran imejitolea kuufanikisha mpango wake wa Kinuklia bila kujali hatua zitakazochukuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Iran Pia imeonya kwamba itasimama kidete kutetea haki yake ya kuwa na mpango wa Kinuklia.

Bwana Khamenei amelaani kile alichokiita ni kutumiwa vibaya kwa baraza la usalama na nchi zenye nguvu juu ya mpango wa Nuklia wa nchi yake.