1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI: Mkutano wa kupinga utandawazi waanza nchini Kenya.

20 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCZU

Washiriki zaidi ya elfu themanini wamejumuika leo mjini Nairobi, Kenya katika kongamano la kila mwaka dhidi ya utandawazi.

Washiriki hao wana matumaini ya kukutana na kuandaa mitandao ya wanaharakati itakayowasaidia kukabiliana vilivyo na sera za utandawazi wanazosema zinawatatiza watu masikini.

Kongamano hilo linaloitwa World Social Forum limelengwa kuuonyesha ulimwengu mapambano ambayo yamekuwa yakiendelea barani Afrika dhidi ya kutawaliwa na mataifa ya kigeni, ukoloni pamoja na ukoloni-mamboleo.

Mapema leo asubuhi maelfu ya wanaharakati hao wanaopinga utandawazi waliandamana mjini Nairobi.

Wanaharakati kiasi elfu tano waliandamana mabarabarani tofauti na idadi ya maelfu kadhaa waliotarajiwa kushiriki maandamano hayo.

Kongamano hilo ambalo ni la saba tangu kuanzishwa World Social Forum mwaka elfu mbili na moja, limeandaliwa kwa mara ya kwanza katika bara la Afrika ambalo limeathirika kwa kiasi kikubwa na siasa ya utandawazi.

Maswala makuu yatakayojadiliwa kwenye kikao hicho ni janga la Ukimwi, utatuzi wa mizozo, madeni na pia suala la uhamiaji.

Kongamano hilo litamalizika siku ya alhamisi ijayo.