1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani wako nyuma ya mashambulio ya Boston?

17 Aprili 2013

Mashambulio ya mabomu ya Boston,serikali ya kisoshialisti ya Ufaransa na juhudi za kurejesha nidhamu,na kuundwa chama kipya nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/18HHk
Mabaki ya chombo kilichotumiwa kuripuwa mabomu huko BostonPicha: Reuters

Tuanzie lakini Marekani ambako juhudi za kuwasaka waliohusika na mashambulio ya mabomu ya Boston zimeshika kasi.Gazeti la "Darmstädter Echo" linaandika:

Mshambuliaji au washambuliaji wa Boston walitaka kuuwa na kuwaathiri watu wengi zaidi.Uhalifu huo ni uhaini mkubwa kwasababu umetokea katika ule wakati ambapo wanaspoti au familia zao walikuwa wakifurahikia kufika ufundoni mwa mbio zao za marathon. Vipi Marekani inakabiliana na kishindo hiki  cha shambulio la kigaidi,itategemea na jibu la suala:nani walikuwa nyuma ya kuzipaka damu mbio za marathon za Boston.

Bado haijulikani nani walikuwa nyuma ya mashambulio ya mabomu ya Boston.Hata hivyo gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linahisi:

Yasisahauliwe makundi yote ya siasa kali za mrengo wa kulia yaliyoko nchini Marekani..Au wanaharakati wanaopigania haki ya kumiliki silaha na ambao hatua yoyote ya kubatilisha sheria hiyo wanaiangalia kuwa sawa na kuendewa kinyume uhuru wa kila raia.Timothy McVeigh aliliripua jengo lote mwaka 1995 huko Oklahoma na kuwauwa watu 168 eti kwasaabu hakutaka kupokea amri kutoka serikalini.Pengine mhusika au wahusika wa mashambulio ya Boston walishawishiwa na hoja kama hizo.Na maandalizi kama haya ya mbio za maradhon za Boston yanayowavutia umati wa watu yanawapa nafasi ya kutajwa na vyombo vya habari.

Sifa ya wasoshialisti yachujuka Ufaransa

Frankreich Präsident Hollande Korruption Vertrauensverlust
Rais wa Ufaransa Hollande ,hamkani ,baada ya kufichuliwa kashfa ya waziri wake wa zamani wa bajeti,Jérôme CahuzakPicha: Reuters

Kashfa iliyozushwa na waziri wa zamani wa bajeti wa Ufaransa aliyeficha kwa muda wa miaka 20 hakuwa akilipa kodi ya mapato - amehamishia miliki yake katika benki za Uswisi na baadae Singhapore,Jérôme Cahuzac ingali bado inaitikisa nchi hiyo.Rais Francois Hollande amewataka wanachama wote kuanzia wa bunge hadi wa serikali wafichue rasmi wanachokimiliki.Jee hatua hiyo itasaidia kurejesha nidhamu na imani ya wananchi?Gazeti la "Die Welt linaandika:

Kwa kuwataka mawaziri wake waweke wazi wanachokimiliki,Francois Hollande ametaka kuwagutuwa mawaziri wawe waadilifu.Baada ya zahma iliyosababishwa na waziri wa zamani wa bajeti Jérôme Cahuzak aliyekuwa na acaunti za siri nchini Uswisi,kipa umbele kwa rais Hollande ni kurejesha imani ya wananchi.Hata hivyo lengo hilo bado hajalifikia.Na mawaziri wake amewadhoofisha kwasababu hivi sasa wanaangaliwa kama matajiri licha ya kutokea mrengo wa shoto na wengine wanaangaliwa kama malofa.

Chama kipya ni changamoto

Partei Alternative für Deutschland AfD
Konrad Adam(kushoto),Frauke Petry (kati) na Bernd Lucke wakifurahikia kuteuliwa wote watatu kukiongoza chama kipya "Chama mbadala" kwa Ujerumani."Picha: picture-alliance/dpa

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kishindo cha kuundwa chama kipya "Chama mbadala kwa Ujerumani"-AfD.Gazeti la "Südkurier "linaandika

"Tutoke katika kanda ya Euro" hiyo ndio kauli mbiu ya chama mbadala kwa Ujerumani.Chama hicho ni kishindo hasa kwa vyama ndugu vya CDU/CSU na waliberali wa FDP.Sawa na chama "die Piraten" au maharamia,na hiki kipya pia kinawalenga wale waliovunjika moyo.Lakini kama idadi yao itatosha kuwaingiza bungeni maharamia wepya wanaofunga tai ,hakuna ajuae.Litakuwa pigo kubwa lakini kwa vyama vinavyounda serikali ya sasa ya muungano mjini Berlin,hata kama chama mbadala kwa Ujerumani kitajikingia asili mia tatu tu za kura uchaguzi mkuu utakapoitishwa september mwaka huu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman