1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Baraza la Usalama lataka Umoja wa Afrika upeleke majeshe haraka Somalia.

3 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCVd
Rais wa mpito wa Somalia Abdillahi Yusuf
Rais wa mpito wa Somalia Abdillahi YusufPicha: AP

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito kwa Umoja wa Afrika upeleke haraka iwezekanavyo vikosi vyake vya kulinda amani nchini Somalia ili Ethiopia iondoe majeshi yake nchini humo na pia serikali hiyo ya mpito ipate kufutilia mbali hatua za dharura za usalama ilizotangaza.

Baraza hilo lenye nchi kumi na tano wanachama, jana, pia lilipendekeza Umoja wa Mataifa kuharakisha kupeleka ujumbe wake wa kiufundi nchini Somalia kutathmini na kutoa mapendekezo kuhusu mahitaji ya kiusalama ya siku za usoni ya nchi hiyo.

Vikosi vya serikali ya mpito vikisaidiwa na majeshi ya Ethiopia viliwafurusha wanamgambo wa Kiislamu baada ya kukabiliana nao kwa majuma mawili mwishoni mwa mwaka uliopita.

Hata hivyo mji mkuu Mogadhishu na maeneo mengine kadhaa nchini humo yamekuwa yakikabiliwa na ghasia hadi ya Umoja wa Afrika kujitolea kupeleka majeshi ya kulinda amani kabla ya Ethiopia kuondoa vikosi vyake nchini humo.

Tangu waliposhindwa wanamgambo wa kiislamu wametawanyika katika eneo la kusini mwa Somalia na pia nchini Kenya na baadhi yao wameapa wataendesha vita vya kuvizia vya muda mrefu.

Wanamgambo hao wa Kiislamu wanapinga majeshi ya Umoja wa Afrika kupelekwa nchini humo.