1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New York. Bashir atoa ishara ya kukubali jeshi la UM.

28 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCfZ

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limeukaribisha kwa tahadhari uamuzi uliotolewa na rais wa Sudan Omar Al-Bashir wa kukubali kuwekwa kwa jeshi la pamoja kati ya umoja wa mataifa na Afrika katika jimbo la magharibi ya Sudan la Darfur.

Jeshi hilo litakuwa sehemu ya mpango wa umoja wa mataifa wenye awamu tatu unaolenga katika kumaliza ghasia katika jimbo la Darfur.

Kufuatia mkutano wa faragha wa baraza la usalama , katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan amesema kuwa anatiwa moyo na mtazamo wenye mwelekeo sahihi wa rais Bashir katika barua yake.

Wanadiplomasia kadha , hata hivyo, wameeleza wasi wasi wao, wakisema Sudan imeshindwa kutimiza majukumu yake hapo kabla. Bashir hapo kabla alikataa kuruhusu jeshi lolote la umoja wa mataifa kuingia katika jimbo la Darfur.

Kiasi watu 200,000 wameuwawa na wengine zaidi ya milioni 2 wamekimbia makaazi yao tangu mzozo huo uanze katika jimbo hilo mapema mwaka 2003.