1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Marekani yawasilisha azimio jipya la tume ya kulinda amani kusini mwa Sudan

24 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC7U

Marekani inataka kutumia azimio la Umoja wa Mataifa kurefusha muda wa tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika eneo la kusini mwa Sudan. Lengo la hatua hiyo ni kuongeza mbinyo wa kupelekwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika jimbo la Darfur.

Lakini pendekezo la azimio hilo la Marekani huenda likabiliwe na upinzani mkali kutoka kwa wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wanaotaka juhudi za kulinda amani kusini mwa Sudan zisijumulishwe na juhudi za kuunda kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani Darfur.

Azimio hilo litarefusha muda wa kikosi cha Umoja wa Mataifa katika eneo la kusini kwa miezi mitatu hadi tarehe 31 mwezi Julai mwaka huu.

Akizungumza kuhusu hali nchini Sudan balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, Emyr Jones Parry, amesema cha muhimu ni kujaribu kupunguza matatizo nchini humo.

´Darfur kwa upande mmoja, eneo la kusini na maeneo mengine ya Sudan; yote ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuheshimu mipaka ya nchi hiyo na kujaribu kuchangia kupunguza matatizo yake yote.´

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, amewaambia wandishi wa habari mjini New York kwamba pendekezo la azimio lililowasilishwa na Marekani linatakiwa kurekebishwa.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litalijadili pendekezo hilo wiki ijayo.