1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Umoja wa Mataifa kutanuwa shughuli zake Iraq

11 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBaH

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekubali kuongeza muda wa shughuli za Umoja wa Mataifa nchini Iraq.

Azimio hilo ambalo limewasilishwa na Marekani na Uingereza limeidhinishwa kwa kauli moja na nchi 15 wanachama wa baraza hilo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ameridhika na kuongezwa muda kwa mwaka mmoja shughuli za usaidizi za Umoja wa Mataifa nchini Iraq zinazojulikana kwa ufupi kama UNAMI ambazo muda wake umemalizika hapo jana.

Ki-moon anasema Umoja wa Mataifa umejizatiti hasa kuwasaidia wananchi wa Iraq na anaridhika kuwa na fursa hivi sasa ya kuonngeza michango yao pale inapowezekana katika fani muhimu kama vile usuluhishi wa taifa,mazungumzo ya kanda, msaada wa kibinaadamu na masuala ya haki za binaadamu.

Licha ya kuruhusu wafanyakazi zaidi wa UNAMI kuwepo Iraq azimio hilo linafunguwa njia ya kuwepo kwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Iraq ili kusaidia serikali ya Iraq.

Baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakipinga kutanuliwa kwa shughuli hizo kutokana na kuendelea kwa umwagaji damu nchini humo.