1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nuri Sahin ndiye nyota wa Bundesliga

23 Mei 2011

Mchezaji wa timu bingwa Borussia Dortmund, Nuri Sahin, amechaguliwa kuwa mchezaji bora kwa msimu 2010/2011 kwenye ligi ya Ujerumani, Bundesliga.

https://p.dw.com/p/11MCQ
Nuri Sahin wa Borussia DortmundPicha: dapd

Baada ya kukamilika msimu wa ligi ya Ujerumani, Bundesliga, mchezaji nyota Nuri Sahin ambaye ni Mjerumani mzaliwa wa Uturuki, na anaeihama timu bingwa msimu huu, Borussia Dortmund, na kujiunga na timu ya Uhispania, Real madrid, amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu wa mwaka 2010 -2011.

Fußball-Profi Nuri Sahin Wechsel nach Spanien
Nuri SahinPicha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa gazeti la Kicker, mchezaji huyo wa kiungo cha kati mwenye umri wa miaka 22, alipokea kura asilimia 46.1 na akafuatia nyuma na mchezaji mwenza katika timu hiyo bingwa, Mario Goetze, akiwa na asilimia 18.7. Hii ni kwa mujibu wa utafiti iliofanya gazeti hilo miongoni mwa wachezaji 298.

Arturo Vidal kutoka Chile na anayeichezea timu ya Bayer Leverkusen ameichukuwa nafasi ya tatu akifuatwa na mchezaji wa Bayern Munich kutoka Uholanzi, Arjen Robben, na mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Mario Gomez, katika nafasi ya tano.

Kipa wa Schalke anayetazamiwa na wengi kuihama timu hiyo na kujiunga na Bayern Munich, Manuel Neuer, amechaguliwa kuwa kipa bora zaidi kwa kujipatia asilimia 70.

Na kocha Jurgen Klopp wa Dortmund alichaguliwa kuwa kocha bora kwa mafanikio yake ya kuiongoza timu hiyo kuchukuwa ubingwa wa Bundesliga msimu huu, ambao ni wa kwanza tangu walipounyakuwa wao wa mwisho, msimu wa mwaka 2001- 2002.

DFB Pokal - Kombe la Ujerumani

Kwengineko Schalke 04 ilifanikiwa kujinyakulia kwa mara ya tano taji la Ujerumani kufuatia kipigo walichoipa timu iliopo kwenye divisheni ya pili, Duisburg, na imefuzu sasa kujikatia tiketi kwa mashindano ya ligi ya Ulaya.

Ulikuwa ushindi wenye pengo kubwa kwa Schalke katika kuwania kombe hilo tangu mwisho timu hiyo ilipoifunga Kaiserslautern mabao kama hayo mnamo mwaka 1972.

DFB-Pokalfinale 2011 MSV Duisburg - FC Schalke 04
Sherehe baada ya ushindiPicha: dapd

Mchezaji chipukizi wa Schalke, Julian Draxler, alisukuma tobwe la kwanza kunako dakika 18, na dakika nne baadaye mholanzi Klaas Jan Huntelaar aliongeza la pili baada ya kupokea pasi safi kutoka kwake Jefferson Farfan, ambaye baadaye tena alitoa pasi nyengine ya kona kwa Benedikt Hoewedes aliesukuma hedi wavuni kunako dakika 42 ya awamu ya kwanza, na kuipa Schalke uongozi mkuu dhidi ya Duisburg.

Akirudi kwa nguvu mpya, Huntelaar alimsukumia mpira Jurado kuongeza la nne mapema katika awamu ya pili, na baadaye yeye mwenyewe kufunga la lala salama, kufuatia uzembe uliotokea katika ulinzi wa Duisburg.

Na pengine maneno yatakayokumbukwa katika ushindi huo ni yale ya mkurugenzi wa michezo wa Schalke, Horst Heldt, aliyesema,'Tunajivunia timu hii'.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Afpe/rtre
Mhariri:Othman Miraji