1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olmert kukutana na mfalme Abdullah II wa Jordan

Josephat Charo15 Mei 2007

Mfalme Abdullah II wa Jordan na waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, wanakutana leo kujadiliana juhudi za kutafuta amani ya Mashariki ya Kati. Wakati huo huo, Wapalestina takriban saba wameuwawa kwenye shambulio huko Gaza.

https://p.dw.com/p/CHEN
Machafuko katika barabara za Gaza
Machafuko katika barabara za GazaPicha: AP

Waziri mkuu wa Israeal, Ehud Olmerta amesema leo mjini Petra nchini Jordan kwamba yuko tayari kukutana na viongozi wa mataifa ya kiarabu wasio na msimamo mkali wa kidini. Lengo la mkutano huo litakuwa kuujadili mpango wa amani uliofufuliwa mwezi Machi mwaka huu kwenye mkutano wa mjini Riyadh, Saudi Arabia lakini hakuna masharti yanayotakiwa kuwekwa kabla ya mkutano huo.

´Ninawakaribisha viongozi 22 wa mataifa ya kiarabu walio tayari kuwa na amani na Israel waje wakati wowote wakitaka, wakae pamoja nasi watuambie mawazo yao´, amesema Ehud Ehud kabla kukutana na mfalme Abdulla wa Jordan. Aidha Olmert amewaambia washindi wa tuzo la amani la Nobel katika mji wa kale wa Petra kuwa ikiwa viongozi wa kiarabu watashindwa yeye binafsi yuko tayari kukutana nao mahali popote.

Mkutano kati ya Ehud Olmert na mfalme Abdullah II wa Jordan unafanyika wakati mchakato wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati ukiwa umegubikwa na hali ngumu ya kisiasa inayomkabili waziri mkuu Ehud Olmert. Olmert anakutana kwa mara ya kwanza na kiongozi wa kiarabu tangu mkutano wa kilele wa mjini Riyadh.

Jumuiya ya nchi za kiarabu imezitaka Misri na Jordan, nchi pekee za kiarabu zilizosaini mikataba ya amani na Israel, ziishawishi Israel iukubali mpango wake mpya wa amani. Mfalme Abdullah II amekuwa akiendeleza juhudi za kidiplomasia kuufanikisha mpango huo. Siku moja kabla kukutana na Ehud Olmert, mfalme Abdullah II alimtaka makamu wa rais wa Marekani, Dick Cheney, asaidie kuzifufua juhudi za kutafuta amani ya Mashariki ya Kati ambazo zimekwama.

Sambamba na ripoti hiyo, maafisa takriban saba wa polisi wameuwawa mapema leo katika Ukanda wa Gaza. Mauaji hayo yametokea wakati wanamgambo wa chama cha Hamas walipokivamia kikosi cha maafisa wa polisi wa chama cha Fatah kwenye kituo cha upekuzi cha mpakani kati ya Gaza na Israel. Hapo awali msemaji wa Hamas, Ghazi Hamad, alisema wamefikia makubaliano ya kukomesha machafuko.

´Naweza kuthibitisha kwamba kupitia mikutano kati ya waziri mkuu na viongozi wa Hamas na Fatah, tumefikia makubaliano ambayo sharti yatekelezwe. Kwanza rais ameamuru vikosi vyote vya usalama viondoke kutoka barabarani na nadhani viongozi wa Hamas na Fatah pia wameamuru vikosi vyao viondoke na vikomeshe machafuko na mapambano.´

Ghazi Hamad alisema walikubaliana pia mateka wote wanaozuiliwa waachiliwe huru. ´Watu wote waliotekwa nyara wanatakiwa waachiliwe huru na tabia ya kuchochea vyombo vya habari ikome. Na nadhani tulichokifanya ni hatua muhimu ya kukomesha aina yoyote ya hali ya wasiwasi katika barabara za Palestina.´

Shambulio dhidi ya kikosi cha Fatah limeelezwa kuwa baya zaidi kuwahi kufanywa tangu mapigano baina ya wafuasi wa Hamas na Fatah yalipozuka siku tatu zilizopita ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ya mamlaka ya Palestina.