1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OSLO : Mvutano wa makombora ya kujihami wapamba moto

27 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC6g

Mzozo kutokana na mipango ya Marekani ya kuweka kambi za makombora ya kujihami Ulaya ya mashariki umepamba moto hapo jana wakati Urusi ilipositisha majukumu yake katika mkataba wa ulinzi barani Ulaya uamuzi ambao umezusha wasi wasi mkubwa miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Magharibi.

Katika mjadala mkali wa NATO mjini Oslo Norway Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov ameonya kwamba Urusi itakomesha majukumu yake katika mkataba wa vikosi vya wanajeshi wa kawaida barani Ulaya iwapo nchi wanachama wa NATO hazitouidhinisha mkataba huo.Kauli yake hiyo inakuja baada ya Rais Vladimir Putin wa Urusi kutowa wito katika hotuba ya taifa kwenye televisheni wa kusitishwa kwa majukumu ya Urusi kwenye mkataba huo kutokana na mipango ya Marekani kuweka makombora ya kujihami katika nchini Poland Czeck.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeir amesema ni muhimu kwa Ulaya kuzuwiya kufumuka kwa tuhuma kati ya Mrekani na Urusi na kwamba hatua yoyote ile ya kusitishwa kwa majukumu juu ya mkataba huo wa silaha ni hatua yenye kuelekea kwenye upande usio sahihi.

Amesema kile wanachohitaji ni upunguzaji na udhibiti zaidi wa silaha.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice amerudia tena kusema kwamba mpango huo wa Marekani wa kuweka makombora ya kujihami Ulaya ya mashariki hauilengi Urusi na ameuita wasi wasi wa Urusi kuwa ni upuuzi.