1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa atembelea mji wa kihistoria wa Erfurt

23 Septemba 2011

Leo hii (23.09.2011), Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Benedict XVI anatembelea mjin wa kihistoria wa Erfurt, ambako anaongoza misa maalum ya kanisa lake na makanisa ya kiinjili ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/12f9X
Baba Mtakatifu Benedict XVI
Baba Mtakatifu Benedict XVIPicha: dapd

Misa hii ya pamoja inatajwa kuwa ya aina yake, kwani inafanyika katika kanisa lile lile la Augustine ambalo karibu miaka 500 iliyopita, mtawa na msomi wa Kijerumani, Martin Luther, aliposali kabla ya kutangaza uasi dhidi ya Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, wakati huo yakiongoza dola ya Roma.

Siku yake hii ya pili ya ziara ya Papa, imeanza kwa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, kukutana na Baraza la Waislamu la Ujerumani, baada ya hapo jana kukutana na viongozi wa Kiyahudi kabla ya kuendesha misa kubwa katika uwanja wa mpira jijini Berlin iliyohudhuriwa na waumini 70,000.

Katika mkutano wake na viongozi wa Waislamu, Baba Mtakatifu alihimiza juu ya Wakristo na Waislamu kufanyia kazi yale mambo yanayowaunganisha katika imani zao ili kujenga ulimwengu ulio bora zaidi.

"Tunaweza kuonesha ushuhuda muhimu katika maeneo mengi muhimu ya maisha kwenye jamii zetu", Baba Mtakatifu aliwaambia wawakilishi hao 15 wa jumuiya za Kiislamu, wakfu na walimu wa dini hiyo, na kupigia mifano ya ulinzi wa familia uliojikita kwenye ndoa, heshima kwa uhai katika kila hatua ya kimaumbile na ushajiishaji wa haki za kijamii.

Waumini wakishiriki misa kwenye uwanja wa Olimpiki wa Berlin iliyoendeshwa na Baba Mtakatifu XVI, tarehe 22 Septemba 2011.
Waumini wakishiriki misa kwenye uwanja wa Olimpiki wa Berlin iliyoendeshwa na Baba Mtakatifu XVI, tarehe 22 Septemba 2011.Picha: dapd

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huu ni mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Ujerumani, Aiman Mazyek na pia wajumbe wa Umoja wa Kiislamu wa Uturuki unaojihusisha na mambo ya dini, DITIB. Kiasi ya Waislamu milioni nne wanaishi Ujerumani, asilimia 45 kati yao wakiwa ni raia wa Ujerumani.

Aiman Mazyek amesema kwamba Baba Mtakatifu ameweka umuhimu wa pekee katika mdahalo baina ya Wakritsto na Waislamu, jambo ambalo viongozi wa Kiislamu wanalichukulia kuwa ni fursa adhimu.

"Lazima tuweke wazi kwamba tukiwa na sauti moja, kwamba kuchupa mipaka na kufanya chochote kilicho nje ya itikadi kinyume cha maumbile ya kibinaadamu, dhidi ya hoja za kiikolojia na kiuchumi". Amesema Mazyek.

Hapo jana jioni katika hotuba yake kwenye Bunge la Ujerumani, Baba Mtakatifu aliwataka wanasiasa kutokuyatolea muhanga maadili yao kwa kupapia nguvu za kisiasa.

"Siasa lazima iwe msingi wa kujenga haki na hivyo msingi wa amani pia. Bila ya shaka wanasiasa huwa wanatafuta mafanikio, lakini asiyekuwa na moyo wa uadilifu na haki hawezi kuwa mwanasiasa mzuri. Maana mafanikio ya kweli ni kuwepo kwa uadilifu, dhamira ya haki na ufahamu wa haki za wengine." Baba Mtakatifu aliwaambia wabunge wa Ujerumani.

Baba Mtakatifu Benedict XVI ni Mjerumani kwa asili yake na ni Ujerumani hii hii, ambayo uasi dhidi ya Kanisa Katoliki kwenye mji wa Erfurt hapo mwaka 1517 ulisababisha kumeguka kwa kanisa hilo na kuzaliwa makanisa ya kiinjili, likiwemo kanisa la Kiluteri.

Msuguano huu baina ya Kanisa Katoliki na makanisa ya Kiinjili ni mada muhimu hadi leo nchini Ujerumani, na moja kati ya sababu zinazowafanya wengine kuigomea ziara hii.

Zaidi ya wabunge 100 waliigomea hotuba yake Bungeni hapo jana, huku zaidi ya watu 9,000 wakiandamana kupinga msimamo wa Kanisa Katoliki katika masuala ya utoaji mimba, dhima ya mwanamke, ushoga, kashfa za ngono na matumizi ya kondomu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AP/AFP
Mhariri: Josephat Charo