1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa atoa mwito wa amani.

Charles Mwebeya9 Aprili 2007

Kiongozi wa kanisa la Catholic Papa Benedict wa 16 ametoa wito wa amani duniani , na kuelezea kufadhaishwa kwake na hali ya machafuko mashariki ya kati, katika ujumbe wa Pasaka alioutoa hapo jana katika viwanja vya kanisa la mtakatifu Peter huko Vatican.

https://p.dw.com/p/CB4q
Papa Benedikt wa 16 akitoa ujumbe wa Pasaka katika viwanja vya kanisa la mt.Peter , Vatican
Papa Benedikt wa 16 akitoa ujumbe wa Pasaka katika viwanja vya kanisa la mt.Peter , VaticanPicha: AP

Katika ujumbe huo , Papa Benedict wa 16 akizungumza katika lugha mbalimbali ,ameelezea kutofurahishwa kwake na mauaji yanayoendelea huko mashariki ya kati na hususani nchini Iraq na Afghanstan.

Amesema hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana kutokana na juhudi za usalama huko Iraq , bali kinachoendelea ni mauaji na watu kuikimbia nchi hiyo.

Lakini Papa Benedicto wa 16 , alionyesha matumaini yake katika eneo la mashariki ya kati kutokana na mazungumzo yanayoendelea hivi sasa kati ya Israel na mamlaka ya Palestina.

Mazungumzo kati ya Israel na mamlaka ya Palestina yameendelea , licha ya Israel kuikataa serikali ya umoja wa kitaifa , inayojuimuisha kundi la Hamas.

Vilevile amezungumzia wasiwasi wake juu ya hatma ya kisiasa nchini Lebanon na kusema nchi hiyo inakabiliwa na hatari kubwa katika siku za usoni.

Kiongozi huyo wa kanisa katoliki ameeleza wasiwasi mkubwa juu ya dhiki kubwa katika nchi zinazoendelea na mabaa ya njaa, magonjwa na vita pamoja na matumizi ya nguvu yanayohalalishwa kwa sababu za kidini.

Akizungumzia Bara la Afrika na Asia , Papa ameelezea kusikitishwa kwake na ukiukwaji wa haki za binaadam pamoja na machafuko katika baadhi ya nchi.

Amesema ana wasiwasi mkubwa juu ya hali ilivyo katika eneo la Darfur na machafuko pamoja na uharamia katika jamhuri ya kidemokrasi ya watu wa Kongo.

Vilevile Ujumbe wa papa uligusia hali nchini Zimbabwe na Somalia, kama nchi zilizokumbwa na matatizo makubwa ya kisiasa na kiuchumi.

Mbali na ujumbe huo wa pasaka , maelfu ya waumini walisherehekea sikukuu hiyo katika nchi mbalimbali duniani.

katika visiwa vya Solomon, waumini walienda makanisani kuwaombea wahanga wa tetemeko la Tsunami, ilhali misa nyingine kama hiyo, ikifanyika katika kanisa kubwa la dhehebu la katoliki nchini Ufilipino.

Huko Timor ya mashariki , nchi yenye wafuasi wengi wa madhehebu ya katoliki, maelfu ya waumini walionekana wakielekea makanisani kuombea amani ya nchi hiyo , inayofanya uchaguzi wake mkuu hii leo.

"Kutokana na Pasaka inabidi tukatae ghasia. Natoa mwito kwa wagombea wote kukubali matokeo ya uchaguzi huu" alisema Rais wa nchi hiyo anayemaliza muda wake Shanana Gushmao.

Naye Askofu mkuu wa Cantebury, Rowan Williams wa kanisa la Anglikan, amewaasa wafuasi wake kuwa tayari kukubali maridhiano na kusamehe, kama njia kuu ya kutatua mizozo hususani katika ngazi za kimataifa.

Nchini Ukraine mamia ya watu walisherehekea siku kuu ya Pasaka kwa maandamano dhidi ya Rais Viktor Yushenko, wakiwa na keki na mayai yenye rangi ya chama cha waziri mkuu Viktor Yanukovich, ambaye amekataa agizo la Rais Yushenko la kuvunja bunge.

Siku kuu ya pasaka ni siku takatifu katika kalenda ya dini ya kikristo , ikiadhimisha ufufuko wa Bwana Yesu Kristo .